Manchester, England.
Kocha Louis Van Gaal ameendelea kukumbana na wakati mgumu Manchester United baada ya hapo jana usiku kuzomewa na mashabiki wa klabu hiyo katika mchezo wa kundi B wa ligi ya mabingwa dhidi ya CSKA Moscow.
Van Gaal alikumbwa na kisanga hicho kipindi cha pili cha mchezo baada ya kufanya mabadiliko kwa kumtoa Antony Martial na kumuingiza Marouane Fellaini mabadiliko yaliyowakera mashabiki na kuanza kumzomea kwa madai kuwa wamechoshwa na soka la kujihami la kocha huyo Mdachi ambaye kabla ya ushindi wa jana alikuwa ameiongoza Manchester United kwa dakika 404 bila kufunga bao lolote.
Je,Van Gaal anasemaje?
Van Gaal amewaambia mashabiki hao kuwa yeye siyo kiziwi na kuwa ameisikia zomea zomea ile lakini amewataka mashabiki hao kutokatishwa tamaa na maamuzi yake.
Achapia jina la Smalling
Akionekana mwenye furaha baada ya kuilaza CSKA Moscow kwa bao 1-0 na kukalia kiti cha uongozi wa kundi B,Van Gaal alijikuta akimuita mlinzi wake Michael Smalling badala ya Chris Smalling wakati akimwagia sifa mlinzi huyo wa England kufuatia kuokoa mpira wa straika wa CSKA Moscow Seydou Doumbia uliokuwa unaelekea langoni.
Hii ni mara ya pili kwa Van Gaal kuchapia jina la mlinzi huyo mara ya kwanza ikiwa ni mwezi julai katika ziara ya kujiandaa na msimu mpya huko Marekani alipomuita Mike badala ya Chris.
0 comments:
Post a Comment