Dar es Salaam,Tanzania.
Uongozi wa klabu ya Azam umemshtaki kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) winga wake
Brian Majwega kwa madai ya kujiunga na Simba akiwa bado na mkataba.
Azam, pia imesema kuwa haina mpango wa kumuuza au kumtoa kwa mkopo
mshambuliaji Didier Kavumbagu anayetakiwa na Simba.
Kwa sasa, Kavumbagu anaichezea Burundi ‘Intamba Murugamba’ kwenye
mashindano ya Kombe la Chalenji nchini Ethiopia.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba jana alisema kuwa Majwega
hakuitendea haki klabu hiyo kwani katika mkataba wa miaka miwili, ametumikia
kwa miezi mitatu pekee.
Kawemba alisema kuwa hawana haja ya malumbano na mchezaji huyo wala
Simba, kwani wao wanajua nini wanafanya na ndiyo maana wameamua kuchukua hatua stahiki.
Alisema kuwa walitoa taarifa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kuhusu vitendo vya mchezaji huyo na wao
kuendelea kufuatilia kwa karibu hadi kufikia hatua ya kuwaruhusu kusajili mchezaji mwingine, wakisubiri hatima yake.
“Sisi ni watu makini, tunajua
kinachoendelea, kwa Simba kuwatumia wachezaji wao wenye mkataba si mara ya
kwanza, waliwahi kumtumia Ramadhan “Chombo” Redondo katika mechi za
kirafiki huku wakijua wanafanya makosa,
kinachoendelea sasa si cha ajabu kwetu,tena kwa klabu ya Simba,” alisema Kawemba.
Alisema kuwa wanaamini kwa hatua walizochukua, itakuwa fundisho kwa wachezaji wenye tabia kama ya Majwega aliyetoroka kutoka Azam.
“Nadhani mashabiki wa soka wataona mabadiliko katika hatua za kinidhamu za Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa),mara nyingi klabu huwa zinapigwa faini kutokana na ukiukwaji wa mikataba ya wachezaji, safari hii nadhani itakuwa tofauti,” alisema Kawemba.
“Wakala wake anajua, hata Majwega mwenyewe anajua kinachoendelea,alijaribu kujiunga na KCCA ya Uganda
ikashindikana, kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Uganda, Milutin Sredovic ‘Micho’amekataa kumtumia kutokana na hali ilivyo sasa, sijui kwa upande wa Simba ambao wamemkaribisha mazoezini,”alisema.
Kuhusiana na Kavumbagu, Kawemba alisema kuwa Simba ambayo inatajwa
kutaka kumsajili, ibadili mwelekeo kwani wao hawana mpango wa kumuuza au
kumtoa kwa mkopo.
Alisema kuwa Kavumbagu alikuwa na matatizo wa kifamilia na hakuwa vizuri
kipindi cha machafuko ya Burundi.
0 comments:
Post a Comment