Dar es Salaam,Tanzania.
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo imeachana rasmi na
aliyekuwa Kocha Mkuu wake, Stewart Hall, baada ya kufanyika makubaliano
ya pande zote mbili.
Uongozi wa Azam FC inayodhaminiwa
na Benki ya NMB, umechukua hatua
hiyo kufuatia hivi karibuni Hall kutangaza uamuzi wa kuachia ngazi akiweka wazi kuwa amechoka kufundisha soka Tanzania na sasa anataka kwenda kutafuta changamoto
nyingine mpya ya kufundisha soka nje ya nchi.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema mara baada ya kukaa meza moja na Hall wamekubaliana kwa pamoja juu ya ombi lake hilo huku akieleza kuwa kwa sasa kikosi hicho kitakuwa chini ya Kocha Msaidizi Dennis Kitambi.
Alisema Kitambi atakinoa kikosi hicho katika mechi mbili zilizobakia msimu
huu, ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mgambo JKT
itakayofanyika Jumapili hii (Mei 22) pamoja na ile ya fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) watakayokipiga na Yanga Juni 11 mwaka huu.
“Leo tumeachana na Hall kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya kutuomba kuachia ngazi kwa lengo la kutafuta changamoto nyingine
nje ya nchi, wakati tukijipanga kuunda
benchi jipya la ufundi kwa sasa timu itakuwa chini ya Kocha Msaidizi Dennis Kitambi hadi kumalizika kwa msimu huu,” alisema.
Kawemba pia alichukua fursa hiyo kumpongeza Hall kwa mafanikio aliyoipa timu hiyo kwa muda mchache
aliofanya kazi ndani ya Azam FC huku akimtakia kila la kheri katika timu
nyingine atakayokwenda kuifundisha.
“Tunamshukuru Hall kwa mafanikio aliyotupa msimu huu, kwanza kutupa ubingwa wa Kombe la Kagame,kuingia fainali ya Kombe la FA na sasa tukiwa nafasi ya pili kwenye ligi,hii ni rekodi nzuri na tunamshukuru sana kwa hilo na tunapenda kumtakia kila la kheri katika timu nyingine atakayokwenda kufundisha,” alisema.
Rekodi ya Hall Azam FC!!
Kocha huyo raia ya Uingereza aliyeifundisha Azam FC kwa nyakati
tatu tofauti, tokea aanze kibarua hicho Juni mwaka jana anaondoka akiwa
ameinoa timu hiyo katika jumla ya mechi 62 msimu huu, akishinda mara 41, sare 16 na kufungwa mechi tano.
Katika idadi hiyo ya mechi, Hall ameiongoza Azam FC kufunga jumla ya mabao 111 na kufungwa 41, huku
akimaliza mechi bila kufungwa bao lolote (cleensheet) ndani ya michezo 31 pekee.
0 comments:
Post a Comment