728x90 AdSpace

  • Latest News

    Friday, April 07, 2017

    Kocha wa zamani wa Simba SC matatani Ghana,mashabiki wamvaa mazoezini wakimtaka aachie ngazi,awakimbia

                       

    Accra,Ghana.

    KOCHA wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi,Simba SC Mserbia, Zdravco Logarusic jana Alhamisi aliionja joto ya jiwe baada ya mashabiki wenye jazba wa klabu yake ya sasa ya Asante Kotoko kumvaa mazoezini wakitaka aachie ngazi mara moja kuinoa klabu hiyo baada ya mfululizo wa matokeo mabovu.

    Mashabiki hao ambao idadi yao haikutambulika mara moja walifika kwenye uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo wa Adako Jachie uliopo nje kidogo ya jiji la Accra na kuanza kuporomosha matusi ya nguoni pamoja na kufanya fujo zilizopelekea kuharibika kwa programu nzima ya mazoezi ya siku ya jana.

    Mashabiki hao wanamshutumu Logarusic kuwa ameshindwa kufanya kazi yake ipasavyo licha ya klabu yao kufanya usajili wa nguvu msimu huu.Pia wanamshutumu kwa kuachana na mfumo uliozoeleka klabuni hapo wa 4-4-2 na kuamua kutumia mifumo ya 3-5-2 na 3-4-3 ambayo imeshindwa kuipa mafanikio klabu hiyo zaidi ya kuikutanisha na vipigo vya 1-0 na 2-1 kutoka kwa wapinzani wao wakubwa Heart of Oak na Medeama katika siku za hivi karibuni.

    Wameongeza kuwa kocha huyo amekosa mbinu na uwezo wa kuwanoa mabingwa hao mara mbili wa klabu bingwa Afrika.Mashabiki hao wamekwenda mbali zaidi hata kufikia kumuonya kocha huyo kutojihusisha tena na klabu yao vinginevyo watamfanyia kitu kibaya.


    Logarusic ambaye alikuwa akilifuatilia timbwilitimbwili hilo akiwa ndani ya gari lake dogo aliamua kutimka uwanjani hapo baada ya kusubiri kwa dakika 30 bila ya mashabiki hao kuonyesha dalili za kushusha jazba zao.

    Logarusic ambaye alijiunga na Asante Kotoko mwezi Januari mwaka huu kwa mkataba wa miaka miwili amejikuta akiwa kwenye presha kubwa katika siku za hivi karibuni baada ya kushindwa kuipa timu hiyo ushindi kwenye michezo mitatu iliyopita ya ligi kuu ya nchini Ghana.

                     

    Kwa sasa Asante Kotoko iko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ya Ghana ikiwa na pointi 14,pointi mbili nyuma ya vinara wa ligi hiyo Wafa.



    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Kocha wa zamani wa Simba SC matatani Ghana,mashabiki wamvaa mazoezini wakimtaka aachie ngazi,awakimbia Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top