London,England.
ARSENAL imefanikiwa kuinasa saini ya mlinzi wa kushoto wa Schalke 04 ya Ujerumani,Sead Kolasinac kwa uhamisho huru.Hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini kwao Bosnia.
Kolasinac,23,ambaye amebakiza miezi mitatu kumaliza mkataba wake klabuni Schalke 04 amedaiwa kuwa alikuwa kwenye rada za Arsenal kwa kipindi kirefu na kocha Arsene Wenger anamwona mlinzi huyo mzaliwa wa Ujerumani kama mshindani wa kweli wa Mhispania,Nacho Monreal katika nafasi ya ulinzi wa kushoto.
Taarifa kutoka chombo cha habari cha nchini Bosnia cha Reprezentacija anakotokea Kolasinac zinasema tayari mlinzi huyo ameshaingia mkataba wa awali na Arsenal na kuna taarifa kuwa tayari pia ameshachagua namba ya jezi ambayo atakuwa akiivaa msimu ujao.
Kolasinac amekubali kutua Arsenal baada ya kufanya mazungumzo na kocha Wenger ambaye amemuhakikishia kuwa ataendelea kusalia klabuni Arsenal kwa kipindi cha miaka miwili zaidi.
Mwezi Januari uhamisho wa Kolasinac kwenda Chelsea ulikwama katika dakika za mwisho baada ya Shalke 04 kukataa dau la £5.3m kutoka kwa miamba hiyo ya London.
Msimu huu Kolasinac mwenye uwezo wa kucheza pia kama mlinzi wa kati pamoja na kiungo wa ulinzi ameichezea Shalke 04 michezo 31 akiifungia mabao matatu na kutoa pasi (assists) saba za mabao.
Arsenal imeripotiwa kuwa ilifungua mazungumzo ya awali na wawakilishi wa mlinzi huyo tangu mwezi Januari baada ya kupata taarifa kuwa mlinzi huyo amegomea mkataba mpya klabuni Shalke 04 na ataondoka akiwa mchezaji huru ifikapo mwezi Juni.
Mbali ya Arsenal vilabu vingine vilivyokuwa vikimuwania Kolasinac ni pamoja na Juventus,Manchester City na Liverpool.
0 comments:
Post a Comment