London,England
HATIMAYE Arsenal imefanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza ugenini ligi kuu England tangu Januari 14 baada ya Jumatatu usiku ikiwa ugenini Riverside kuchomoza na ushindi wa mabao 2-1dhidi ya wenyeji wao Middlesbrough ambao hawajaonja radha ya ushindi tangu Disemba 17,2016.
Katika mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki 31,298 ilishuhudiwa Alexis Sanchez akiifungia Arsenal bao la kwanza katika dakika ya 42 kwa mkwaju wa faulo ya moja kwa moja na kufanya kikosi hicho kinachonolewa na Mfaransa,Arsene Wenger kiende mapumziko kikiwa mbele kwa bao hilo moja.
Wenyeji Middlesbrough walikianza vyema kipindi cha pili baada ya kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 50 kupitia kwa mshambuliaji wake Mhispania,Alvaro Negredo.Negredo alifunga bao hilo akiunganisha krosi ya Stewart Downing kutoka wingi ya kulia.
Kiungo Mjerumani,Mesut Ozil aliihakikishia Arsenal ushindi baada ya kuifungia bao la ushindi katika dakika ya 71 ya mchezo.Ozil alifunga bao hilo akiwa karibu kabisa ya lango baada ya kupokea pasi safi ya kifua kutoka kwa Aaron Ramsey.
Ushindi huo umeifanya Arsenal ibaki nafasi ya 6 ikiwa imejikusanyia pointi 57 katika michezo 31.Middlesbrough imebaki nafasi ya 19 baada ya kubaki na pointi zake 24 katika michezo 32 iliyocheza mpaka sasa.
0 comments:
Post a Comment