London,England.
SOKA la England limepata pigo kubwa baada ya beki wa zamani wa taifa hilo na timu ya Aston Villa,Ugo Ehiogu kufariki dunia leo Ijumaa kwa mshituko wa moyo.
Jana Alhamisi Ehiogu,44, alipoteza fahamu na kukimbizwa hospitali baada ya kupata shambulio kali la moyo wakati akiwa katika majukumu yake ya kila siku ya kukinoa kikosi cha U23 cha Tottenham Hotspur kabla ya leo Ijumaa kuripotiwa kuwa amefariki.
Kabla ya umauti kumfika,Ehiogu aliichezea Aston Villa zaidi ya michezo 200 kati ya mwaka 1991 na 2000 kabla ya kutimkia Riverside ambapo aliitumikia Middlesbrough kwa miaka saba.Pia aliichezea timu ya taifa ya England michezo minne.
Akiwa na Aston Villa aliiwezesha timu hiyo ya Villa Park kutwaa kombe la ligi mwaka 1994 na 1996 kabla ya mwaka 2004 kutwaa kombe hilo kwa mara ya tatu akiwa na Middlesbrough.
Vilabu vingine alivyowahi kuchezea beki huyo mwenye asili ya Nigeria ni pamoja na West Brom,Leeds United, Rangers na Sheffield United.Alistaafu kucheza soka mwaka 2009.Julai 2014 Ehiogu alijiunga na Tottenham Hotspur na kupewa jukumu la kuwa kocha wa kikosi cha U23 cha timu hiyo.
0 comments:
Post a Comment