Dar Es Salaam,Tanzania.
WACHEZAJI 11 wa Yanga waliobaki Algeria wanatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Saa 8:20 usiku wa leo.
Shukrani kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lililofanya jitihada za kuhakikisha wachezaji hao wanarejea mapema baada ya kuachwa na ndege jana.
Habari ambazo tumezipata kutoka TFF ni kwamba tayari wachezaji hao wamekatiwa tiketi za kurejea kwa ndege ya Emirates kupitia Dubai.
Ndege inatarajiwa kupaa Saa 10;05 jioni kwa saa za huko na Saa 12;05 jioni kwa saa za huku na itafika Dubai Saa 1;00 usiku, ambako wachezaji watapumzika hadi Saa 4:20 watakapounganisha ndege kurejea Dar es Salaam ambako wanatarajiwa kufika Saa 8:20 usiku.
Wachezaji 11 wa Yanga SC pamoja na Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa wamebaki mjini Algiers baada ya kuachwa na ndege ya shirika la Uturuki, kufuatia kuchelewa kufika Uwanja wa Houari Boumediene jana.
Wachezaji hao ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Beno Kakolanya; mabeki; Juma Abdul, Oscar Joshua, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’ na Kevin Yondan, viungo Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na mshambuliaji Donald Ngoma.
Kundi lingine la wachezaji wa Yanga liliondoka jana na ndege ya Emirates pia kurejea Dar es Salaam kupitia Dubai likiwa na wachezaji saba, ambao ni mabeki Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Hassan Kessy, viungo Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Juma Mahadhi na mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe kupitia Dubai.
Katika kundi hilo kuna benchi zima la Ufundi chini ya Kocha Mkuu, Mzambia George Lwandamina, Msaidizi wake, Juma Mwambusi, Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Noel Mwandila pia wa Zambia, kocha wa makipa, Juma Pondamali, pamoja na Meneja Hafidh Ally, Daktari Edward Bavu na Mchua Misuli, Jacob Onyango.
Juzi Yanga ilitolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa mabao 4-0 na Mouloudia Club Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Al-Jaza’ir, Algiers, Algeria katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi.
Kwa matokeo hayo, Yanga imetolewa kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kushinda 1-0 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam wiki iliyopita, bao pekee la kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.
0 comments:
Post a Comment