Madrid,Madrid.
KADI nyekundu ya moja kwa moja,halafu anakosa mchezo mmoja pekee?Umeona wapi hii?Hili ndilo swali ambalo mashabiki wa Barcelona wanajiuliza kwa sasa baada ya nahodha wa Real Madrid,Sergio Ramos kufungiwa mchezo mmoja kwa kosa la kumchezea rafu mbaya staa wao,Lionel Messi Jumapili usiku kwenye mtanange wa El-Classico.
Licha ya kamati ya nidhamu ya chama cha soka cha Hispania (RFEF) kumfungia mchezo mmoja Ramos pamoja na kumlima faini ya Euro 600,mashabiki wa Barcelona wanaona adhabu hiyo ni ndogo sana na imelenga kuipendelea Real Madrid katika kipindi hiki inapopambana na klabu yao kuwania ubingwa wa La Liga.
Mashabiki hao wamekwenda mbali zaidi na kuhoji kwanini Ramos aliyecheza rafu mbaya zaidi na kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja afungiwe michezo michache zaidi ya Neymar aliyefungiwa michezo mitatu baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano na kumpigia makofi mwamuzi wa akiba.
0 comments:
Post a Comment