Na Paul Manjale
Kuna wakati katika maisha haya tunayoishi tunalazimika kufanya maamuzi magumu sana na yenye kuumiza ili tu mambo yetu flani flani yapate kwenda sawa.
Mapema wiki hii kocha Alan Pardew alichukua uamuzi kuhama toka klabu ya Newcastle United na kutua katika klabu ya Crystal Palace yenye makao yake makuu katika dimba la Selhurts Park.Uamuzi ambao wengi wetu tumeuona kama ni mgumu sana kuuchukua kutokana tu na tofauti kubwa iliyopo kati ya vilabu hivi wiwili.
Newcastle United ni klabu kubwa mno kwa Crystal Palace karibu kwa kila kitu.Ukiachana na vilabu vya Manchester United , Liverpool, Manchester
City, Chelsea na Arsenal,Newcastle ni klabu inayofuatia kwa kuwa vizuri kiuchumi na kwa mambo mengine mengi.
Lakini nyuma ya maisha ya Pardew kuna hadithi ya kusikitisha.Akiwa Newcastle Pardew aliungwa mkono na asilimia ndogo tu ya mashabiki.Inasemekana asilimia tano (5%) tu kati ya mashabiki elfu hamsini na moja na ushee wa Newcastle ndiyo waliyomuunga mkono katika kipindi chote cha maisha yake pale St James Park.Pardew hakuwa na sauti katika usajili.Hakushirikishwa pindi timu ilipotaka kuuza au kununua wachezaji.
Mfano mzuri ni katika mauzo ya kiungo Johan Cabaye kwenda klabu ya Paris Saint Germain.Cabaye aliuzwa kinyume na matakwa ya Alan Pardew kitendo kilichosababisha mgogoro mkubwa kati yake na uongozi wa klabu hiyo hasa mmiliki Mike Ashley.
Mgogoro huo uliivuruga sana Newcastle United kiasi cha kupoteza dira na mwelekeo na kujikuta ikiambulia vipigo katika michezo kumi na moja mfululizo ya michuano ya ligi kuu.Je,katika jaribu hili unadhani Pardew alikuwa analala akasinzia?thubuti hata kwa sindano ya ganzi bado maumivu aliyasikia.
Lakini kama alivyoimba msanii Afande Sele katika wimbo wake uitwao ``Ndugu Zangu" kuwa bora ugali na chumvi kwenye amani kuliko bia na nyama choma vitani.Basi ndivyo hata Alan Pardew alivyowaza.Alishachoka kuonekana kuwa anafaidi kumbe ndani utumbo unamkauka kwa wingi wa ngoja ngoja.
Alihitaji kuondoka hakuwaza tena ukubwa wa St James Park wala udogo Selhurts Park.Hakuwaza tena utajiri wa Newcastle wala umasikini wa Crystal Palace.Ubongo wake ulishakaa mguu sawa tayari kwa kuondoka.
Ndiyo maana hakuhitaji dakika nyingi kufikiria pindi Steve Parish mmiliki wa Crystal Palace alipompigia simu na kumwambia anamuhitaji Selhurts Park.
Pardew amekwenda kule ambako anaamini atafanya kazi yake kwa uhuru.Kule ambako atakuwa na sauti katika usajili wa wachezaji.
Kule ambako atasema namtaka huyu,simtaki yule na bado akasikilizwa.Kule ambako mashabiki watalia nae wakati timu haifanyi vizuri na kucheka nae wakati timu inafanya vizuri.
Alan Pardew anarudi nyumbani Selhurts Park.Kule ambako mpaka leo hii anaabudiwa kwa goli lake la dakika za nyongeza lililoipa ushindi Crystal Palace dhidi ya Liverpool katika nusu fainali ya michuano ya kombe la FA.
0 comments:
Post a Comment