728x90 AdSpace

  • Latest News

    Friday, January 23, 2015

    TAMBWE AMPONZA MWAMUZI LIGI KUU

    Siku moja baada ya Klabu ya Yanga kulalamika kudhalilishwa kwa mchezaji wake, Amisi Tambwe katika mchezo wao
    dhidi ya Ruvu Shooting, Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemwondoa kuchezesha mechi za ligi Kuu mwamuzi wa pambano hilo kwa kushindwa kulimudu.

    Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama,mwamuzi huyo Mohammed Theofil ameondolewa kuchezesha ligi hiyo yaTanzania Bara kwa kipindi kilichobaki.

    Katika mchezo huo uliochezwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kusimamiwa na mwamuzi huyo wa kati, timu ya Ruvu Shooting ilionesha mchezo wa kibabe ambapo baadhi ya wachezaji wake walifanya vitendo vya utovu wa nidhamu pasipo kuadhibiwa.

    Mchezo huo ulisababisha mshambuliaji wa Yanga, Tambwe ambaye ni raia wa
    Burundi, kulalamika kwamba
    alidhalilishwa, huku akidai kuumizwa baadhi ya maeneo ya mwili wake na akidai kuwa aliitwa mkimbizi.

    Lakini akizungumza jana akiwa jijini Mwanza, Chama ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Katibu wa Chama cha Soka Kagera, alithibitisha
    kuondolewa kwa mwamuzi Theofil.

    “Ndio, ni kweli tumemwondoa mwamuzi Mohammed Theofil wa Morogoro kwa kushindwa kumudu mchezo huo wa Yanga na Ruvu Shooting,” alisema Chama na kuongeza:

    “Tarehe sita mwezi
    ujao, Kamati (ya Waamuzi) itakutana na kupitia CD ya mchezo pamoja na taarifa
    ya Kamisaa wa mchezo huo na kuchukua hatua zaidi kwa mwamuzi kama itaonekana anastahili adhabu zaidi.”

    Alisema kwa sasa wamechukua hatua ya kumwondoa katika kuchezesha Ligi Kuu
    kwa sababu katika ratiba yao mpya kwa mechi zijazo za Ligi Kuu, mwamuzi huyo alikuwa amepangwa kuchezesha mechi
    nne, hivyo wameona si vyema kumwacha aendelee kuchezesha mechi zaidi.

    “Kwa sasa tumeamua kumwondoa asichezeshe, na kwa hiyo huu ni uamuzi wa dharura kwa sababu tumeona kuwa
    ana mechi nyingine nne ambazo kwa ratiba mpya ya waamuzi alikuwa amepangwa kuchezesha, kwa hiyo tumeona asiendelee na mechi hizo,”alisema Chama.

    Mkuu wa Kitengo cha Habari na
    Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema jana hatua iliyochukuliwa dhidi ya mwamuzi huyo ni ya kwanza kwani wao walipendekeza waamuzi wote
    waliokuwepo katika mchezo huo
    waadhibiwe.

    Pia alisema wanapenda kuona baadhi ya wachezaji waliomdhalilisha Tambwe.wanachukuliwa pia hatua za kinidhamu.

    “Tumefurahi kwa hatua hiyo, lakini tunasema ni ya kwanza, tulipendekeza iwe kwa wote, tunasubiri kauli ya TFF na
    hatua zaidi dhidi ya wengine,” alisema Muro ambaye kesho timu yake inaikabili Polisi Moro mjini Morogoro.

    Miongoni mwa mambo waliyopendekeza juzi ni TFF kuchukua hatua kali dhidi ya
    wale waliohusika kwa utovu wa nidhamu aliyofanyiwa Tambwe kwa kuzingatia sheria na kanuni za soka.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: TAMBWE AMPONZA MWAMUZI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top