James Eduma,Iringa.
CHAMA cha soka cha mkoa wa Iringa,IRFA kimetangaza kuichukua kwa muda timu ya Lipuli FC (Wanapaluhengo) iliyopanda ligi kuu bara msimu huu.
IRFA kupitia kwa mwenyekiti wake mkuu,Cyprian Kuyava imesema imeamua kuichukua timu hiyo baada ya uongozi wake kushindwa kumaliza mgogoro baina yao hali ambayo tayari imeanza kuathiri maendeleo ya timu hiyo.
Ikiwa chini ya IRFA,Lipuli FC itasaidiwa kujiandaa na msimu ujao wa ligi kuu bara ikiwemo kuweka kambi pamoja na kufanya usajili wa wachezaji wapya.Hali ikiwa shwari timu hiyo itarudishwa kwa uongozi husika.
Wakati huohuo Kuyava ameutaka uongozi wa Lipuli FC kupitia kamati yake tendaji kuhakikisha inamaliza mgogoro wake kwa njia ya amani pamoja na kufanya uchaguzi wake mkuu kwa ajili ya kupata viongozi wapya.
Uongozi wa Lipuli FC uliingia kwenye mgogoro baada ya IRFA kumrejesha madarakani mwenyekiti wake,Abuu Changawa Majeki aliyekuwa amesimamishwa kwa utovu wa nidhamu.
0 comments:
Post a Comment