Dar es Salaam,Tanzania.
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm amesema hatakurupuka kwenye kuongeza wachezaji wapya
kwa ajili ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika
(CAF CC).
Yanga iliingia kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola kwa mabao 2-1 ikiwa ni baada ya kushinda kwa mabao 2-0 nyumbani kabla ya kufungwa 1-0 ugenini.
Katika hatua hiyo Yanga iko kundi moja na timu za TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Bejaia ya Algeria na Madeama Sport ya Ghana.
Pamoja na Yanga kubakisha nafasi sita za kuongeza wachezaji wapya kwenye hatua hiyo lakini Pluijm alisema hatazitumia vibaya nafasi hizo kwa
kufanya usajili wa kukurupuka.
“Tayari nina timu nzuri iliyofanya tufike hatua hii, kwa hiyo lazima niwe na imani na hawa na zaidi kubaki na muunganiko wa kitimu.
Nitasajili lakini sitakurupuka,”alisema Pluijm.Alisema wako katika hatua muhimu ambapo kila kitu hakina budi kuangaliwa kwa umakini ili kisiharibu mambo mazuri waliyotumia muda mwingi kuyatengeneza.
“Kama kocha najua mapungufu ya timu yangu, lakini pia najua ubora wa timu yangu ingawa sio kila mapungufu lazima uongeze mchezaji au usajili wachezaji wengi, nitasajili lakini nitakuwa makini katika hilo,” alisema Pluijm.
Yanga itacheza mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi dhidi ya Bejaia ya Algeria Juni 17, Algiers,Algeria.
0 comments:
Post a Comment