BUENOS AIRES, Argentina
KUSTAAFU kwa Lionel Messi kuichezea timu ya taifa ya Argentina,
kumeigeuza nchi hiyo juu chini siku kadhaa zilizopita, taifa lote
likitetemeshwa na habari hizo baada ya Chile kuwafunga tena kwenye
fainali ya Copa America.
Rais wa Argentina, Mauricio Macri, Meya wa Buenos Aires Horacio,
Rodriguez Larreta na gwiji wa soka, Diego Maradona, wamemwomba straika
huyo wa Barcelona kubadili mawazo yake na huenda ujumbe wote unaosambaa
umekuja kupitia mwalimu wa Entre Rios, Yohana Fucks.
Ombi lake limewagusa mamilioni ya mashabiki wa Argentina ambao
wanatamani sana Messi abadili wazo lake la kustaafu soka la kimataifa.
Barua kamili kama inavyosomeka:
Kwako Lionel Messi,
Yawezekana usiisome barua hii. Lakini naiandika, si kama shabiki wa
soka lakini kama mwalimu wa Argentina, kazi ninayoipenda kama
unavyopenda ya kwako.
Ningeweza kukuandikia kuhusu vipaji vyako vya kipekee katika mchezo
maarufu nchini mwetu, furaha ninayopata kuwa na fursa ya kuona kizazi
cha soka na kwa bahati njema kabisa kukushuhudia ukifanya miujiza
dimbani hali kadhalika jinsi unavyokonga nyoyo za mataifa yote duniani.
Kuelezea hayo nitakuwa narudia mambo. Badala yake nataka unisaidie
kutatua changamoto kubwa kuliko uliyokabiliana nayo wewe. Nataka
unisaidie zoezi gumu la kurekebisha tabia za watoto ambao wanakuona kama
shujaa wa soka na mfano wao wa kuigwa.
Haijalishi ni kiasi gani nina mapenzi na ubobezi katika kazi yangu,
siwezi kupokea sifa nzuri sana kutoka kwa wanafunzi wangu kama
ninavyokukubali. Sasa wataona mfano wao wa kuigwa ukikata tamaa.
Nakuomba usiwaridhishe watu dhaifu; wale ambao wamekasirishwa kwa
kushindwa kutimiza ndoto zao maelfu ambazo walishindwa kutimiza kama
wachezaji soka, wale ambao wanazungumzia mapumziko kwa sababu ni jambo
rahisi kutendeka.
Unasikia hili kutoka kwa mwalimu, ambaye licha baina yetu, lakini
nashughulika na tabia za Argentina za kudhani kazi ya mtu mwingine ni
rahisi, kwamba kufunga magoli ni rahisi kama kujenga nyumba au
mustakabali kwa ajili ya mtu.
Ni mtazamo huo unaoangusha wengi au kuzusha hoja za kijinga
zikiambatana na dharau na jazba juu ya ufanisi wa wengine, kuthamini
ushindi tu na kuhesabu makosa kuwa ni kushindwa, makosa hayo hayo ndiyo
yanayotufanya tuwe watu na tuendelee kujifunza.
Tafadhali usiache soka, usiwafanye wachezaji wangu waamini kwamba
nchi hii inajali ushindi tu kwanza. Usiwaonyeshe kwamba hata uwe
umefanikiwa kiasi gani hutaweza kuwafurahisha wengi na usiwafanye
waamini kwamba wanaishi ili kuwafurahisha wengine. Usiwape ujumbe wa
makosa, licha ya kukabiliana na changamoto nyingi hadi umekuwa maarufu
leo hii.
Iwapo mtu kama wewe, mwenye familia inayokuunga mkono, ukiwa na
utajiri na mashabiki wengi, huwezi, wataaminije kwamba wanaweza
kukabiliana na vita hizo nyingi usiku na mchana?
Siwaelezi ni jinsi gani Messi anacheza soka la kuvutia, lakini maelfu
ya mashuti aliyopiga kufanya mazoezi ya kupeleka mpira katika kona
ambayo kipa hawezi kufika. Nawaeleza kuhusu Messi anayepata maumivu ya
kuendelea kukimbiza ndoto zake; Messi ambaye kwa fedha zote alizonazo
amefanikiwa kuwasaidia watoto wenye mazingira magumu. Nawaambia kuhusu
Messi aliyepevuka; baba wa familia na anayefanya kazi muhimu duniani,
mzazi mwema; Messi ambaye anakosa pia penalti, makosa yetu ndiyo
yanayotufanya tuwe wanadamu na hii inadhihirisha kwamba mchezaji bora
hukosea pia.
Usikate tamaa, usitupe fulana yenye rangi za nchi yetu mbali nawe,
fulana hii ya Argentina inatuwakilisha sote. Tafadhali usiwafanye
wanafunzi wangu kuamini kuwa wao ni watu wa kushindwa.
Wanafunzi wangu wanahitaji kuelewa kwamba mashujaa, wawe ni
madaktari, askari, walimu au wacheza soka, ni wale wanaojitolea kwa
ajili ya wengine hata wakijua kwamba hakuna anayewathamini au kuthamini
kile wanachotoa, lakini wakiamini kwamba ushindi utakuwa ni wa wote na
kushindwa kutakuwa juu yao wenyewe. Lakini pamoja na yote hawakomi
kuthubutu. Lakini pia wana ujasiri ndani yao, wanapopambana dhidi ya
kushindwa hata ulimwengu wote ukisema hatutashinda.
Na siku moja watafurahia ushindi mkuu, watafurahia pamoja na changamoto zote walizokabiliana nazo.
Kila mmoja huzungumzia mpira, lakini naamini moyo wako ni thabiti.
0 comments:
Post a Comment