Dar es Salaam,Tanzania.
LICHA ya wachezaji wa TP Mazembe ya DR Congo kutamba kuifunga Yanga katika mchezo wao wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika leo, lakini pia mabosi wa timu hiyo wapo katika rada za kuwanasa nyota wa Wana-Jangwani hao watakaong’ara.
Miongoni mwa wachezaji wa Yanga wenye uwezo wa kutua katika kikosi cha mabingwa hao wa zamani wa Afrika, wapo Wazimbabwe Donald Ngoma na Thabani Kamusoko, lakini pia wazawa kadhaa kama, Geofrey Mwashiuya na wengineo wa kiwango chake.
Yanga na Mazembe wanatarajiwa kuonyeshana kazi leo katika Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mechi ya pili ya hatua hiyo, zikitokea Kundi A.
Kwa mujibu wa Meneja wa TP Mazembe,Frederic Kitengie, licha ya kuja Dar es Salaam kuchukua pointi kutoka mikononi mwa Yanga, pia wapo kwa ajili ya kuangalia wachezaji wengine kama Mbwana Samatta waliyemtwaa hapa nchini walipokujakukipiga na Simba.
Alisema mbali ya benchi la ufundi, wapo watu maalumu waliokuja kuangalia wachezaji wenye uwezo ambao watawafaa.
“Tulikuja kucheza na Simba tukampata Samatta, hivyo leo tumekuja kuumana na Yanga tuna hakika hatutaondoka bila kuona mchezaji anayetufaa, ukizingatia hivi sasa tuna mahitaji makubwa ya wachezaji wapya,”alisema.
Mbali ya Mwashiuya, wengine wenye uwezo wa kukipiga Mazembe ni Deus Kaseke, Simon Msuva, Juma Mahadh, Juma Abdul na wengineo, akiwamo beki wa kati, Kelvin Yondani ambaye hata hivyo umri unaweza kuwa kikwazo kwake.
0 comments:
Post a Comment