Paris,Ufaransa.
MSHAMBULIAJI na winga wa Real Madrid, Mreno Cristiano Ronaldo ametwaa tuzo ya bao bora la Mwaka baada ya bao alilofunga dhidi ya AS Roma mwezi Machi kuchaguliwa kuwa bao bora la mwaka la michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2015/16.
Ronaldo,31,alifunga bao hilo Katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano (16 bora) uliochezwa katika uwanja wa Stadio Olimpico na Real Madrid kushinda kwa mabao 2-0.
Kabla ya kufunga bao hilo Ronaldo alimpiga chenga beki mmoja wa AS Roma akiwa upande wa kushoto wa uwanja kabla ya kuingia ndani na kufyatua mkwaju mkali uliompalaza Alessandro Florenzi na kisha kutinga wavuni ukimuacha kipa,Wojciech Szczesny akiwa hana la kufanya.
Ronaldo ametwaa tuzo hiyo baada ya kupata asilimia 36 ya kura zote zilizopigwa kupitia mtandao wa UEFA.COM akiwabwaga wapinzani wake wa karibu Alessandro Florenzi wa AS Roma,Saul Niguez wa Atletico Madrid, Luis Suarez na Lionel Messi wote wa FC Barcelona.
0 comments:
Post a Comment