Dar es Salaam,Tanzania.
SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF), linatarajia kuwaweka meza moja
vigogo wa Simba na Yanga ili kumaliza sakata la usajili na kibali cha
Hassan Ramadhan ‘Kessy’.
Hatua hiyo imekuja baada ya Yanga kuwasilisha nakala ya barua ikiwa
imeambatanishwa na mkataba wa Kessy na Simba ambao unaonyesha wazi kuwa
ulimalizika Juni 15, mwaka huu na mchezaji huyo alikuwa sahihi kuingia
mkataba mpya na klabu nyingine.
Yanga ilishindwa kumtumia Kessy katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi
A, Kombe la Shirikisho Afrika wakifungwa 1-0 na Mo Bejaia nchini
Algeria baada ya CAF kuomba barua ya kuruhusiwa kwake kuondoka klabu
yake ya zamani, Simba ambayo hawakuwa nayo.
Akizungumza, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema
kuwa iwapo Simba hawatajibu barua hiyo waliyoandikiwa na wapinzani wao
basi watalazimika kuita viongozi wa pande zote mbili na kukaa nao meza
moja.
“Yanga wamepeleka barua Simba ambayo nakala imeletwa TFF na CAF
(Shirikisho la Soka Afrika) hivyo tunasubiri majibu ya Simba wasipojibu
kwa wakati tutawasiliana na pande zote mbili,” alisema.
Katika barua hiyo ya Yanga imeiomba TFF iwasaidie kumwidhinisha beki
huyo kuanza kazi Jangwani ikiwa hadi kesho (Ijumaa) Simba watakuwa
hawajajibu barua hiyo.
Yanga inaamini kuwa kama klabu ya zamani ya Kessy, Simba itagoma
kujibu barua hiyo itakuwa imemaanisha kuwa haina pingamizi kwa staa huyo
kuichezea miamba hiyo Jangwani.
Na iwapo Simba SC watamwekea pingamizi Kessy, watapaswa kuwa na hoja
za pingamizi ambalo litasikilizwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Richard Sinamtwa.
CHANZO:BINGWA
0 comments:
Post a Comment