Delta State,Nigeria.
Kocha na nahodha wa zamani wa Nigeria Stephen Okechukwu Keshi amefariki dunia alfajiri ya kuamkia leo huko Benin.
Emmanuel Ado ambaye ni kaka wa marehemu amesema Keshi,54, amefariki kwa ugonjwa wa moyo unaoitambulika kwa jina la kitaalamu la Cardiac arrest.
Ado ameongeza kuwa tangu Keshi alipofiwa na aliyekuwa mke wake Kate Keshi kwa ugonjwa wa Kansa Desemba 9,2015 alikuwa mtu wa kuomboleza kila siku anadhani hicho ndicho kilichomuua.
Keshi amekuwa mchezaji wa tano kufariki kutoka katika kikosi cha Nigeria kilichotwaa ubingwa wa AFCON mwaka 1994.Wengine ni Uche Okafor,Thompson Oliha, Rashidi Yekini na Wilfred Agbonavbare.
REKODI
Keshi maarufu kama 'Big Boss' ni kocha pekee raia wa Nigeria aliyewahi kutwaa ubingwa wa AFCON pia ni Kocha wa pili kutwaa ubingwa huo akiwa kama kocha na mchezaji.Wa kwaza alikuwa ni Mahmoud El-Gohary wa Misri.
Mwaka 2006 alifanikiwa kuongoza Togo kufuzu fainali za kombe la dunia za Ujerumani lakini kabla ya kuanza kindumbwe ndumbwe hicho alitimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani Otto Pfister.
Keshi alianza kuichezea Nigeria mwaka 1981 akiwa kama beki wa kati,wakati huo akiwa na umri wa miaka 20 kabla ya kubwaga manyanga mwaka 1994.Alifanikiwa kuicheza Nigeria michezo 64 na kuifungia mabao tisa.
0 comments:
Post a Comment