Kigali,Rwanda.
NAHODHA wa timu ya taifa ya Rwanda, Haruna Niyonzima, amekiri yeye na wachezaji wenzake walistahili kuzomewa na mashabiki wao baada ya kuonyesha kiwango kibovu kilichopelekea "Amavubi" kufungwa mabao 3-2 nyumbani na timu ya taifa ya Msumbiji katika mchezo wa kundi H wa kusaka tiketi ya kucheza michuano ya Afcon uliochezwa siku ya Jumamosi katika uwanja wa Amahoro jijini Kigali.
Niyonzima amesema 'Hiki ni kichapo kikubwa sana kwetu hatukukitarajia.Leo (Juzi) hatukujilinda vizuri kama ambavyo imezoeleka tunapokuwa tukicheza nyumbani.
Tunastahili lawama kwa kupoteza mchezo huu muhimu.Tumeshindwa kuifanya kazi yetu ipasavyo.
Mashabiki wana haki ya kutuzomea kwani tumewaangusha kwa kushindwa kuonyesha kiwango bora kama kile tulichokionyesha na kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Mauritius katika mchezo uliopita.
Mchezo ujao tunaenda Accra kucheza na Ghana tutajitahidi tushinde kisha tuone nini kitafuatia'.Alimaliza Niyonzima.
Siku ya Jumamosi mashabiki wa Rwanda waliamua kuizomea timu yao baada ya kufungwa mabao 3-2 na Msumbiji na kufifisha matumaini ya kufuzu michuano ya AFCON kwa mara ya pili baada ya kusubiri kwa miaka kumi na mbili.
Katika mchezo huo mabao ya Msumbiji yalifunga na nahodha Elias Gaspar Pelembe aliyefunga mara mbili pamoja na Apson David Manjate aliyefunga mara moja huku yale ya Rwanda yakifungwa na Jacques Tuyisenge.
0 comments:
Post a Comment