Dar Es Salaam,Tanzania.
MABINGWA wa soka wa Tanzania,Yanga SC leo mchana wameandika historia nyingine mpya na kubwa baada ya kuingia mkataba mnono wa miaka mitano na kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportsPesa yenye makao yake makuu nchini Kenya.
Mkataba huo utaiwezesha Yanga SC kuvuna kitita cha Shilingi Bilioni 5 za Kitanzania katika kipindi cha miaka mitano na kuwapiku mahasimu wao Simba SC ambao Ijumaa iliyopita waliingia mkataba wenye thamani ya Bilioni 4.96 na kampuni hiyo iliyojizolea umaarufu nchini katika siku za hivi karibuni.
Katika mkataba huo Yanga SC itakuwa ikivuna Shilingi Milioni 950 kwa mwaka kwa kuvaa jezi zenye nembo ya kampuni hiyo.Pia mkataba huo utaambatana na motisha (bonasi) ambapo Yanga SC itavuna Shilingi Milioni 100 iwapo itatwaa ubingwa wa ligi kuu msimu ujao na kuendelea.
Yanga SC pia itavuna Shilingi Milioni 250 kama itafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ikiwepo kutwaa kombe la Kagame ambalo hushirikisha timu za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mkurugenzi wa utawala na utekelezaji wa SportPesa, Abbas Tarimba amesema wameamua kuwekeza kwa ajili ya kusaidia na kukuza soka la Tanzania
Mpaka sasa SportPesa imefanikiwa kuvidhamini vilabu vinne vya Kenya na Tanzania ambavyo ni Gor Mahia,FC Leopards,Simba SC na Yanga SC.
SportPesa hajaishia hapo bali pia imejitanua mpaka nchini England ambapo imemwaga pesa kuvidhamini vilabu vya Hull City na Everton.
0 comments:
Post a Comment