Amsterdam,Uholanzi.
PENGINE hii si habari njema sana masikioni mwa mashabiki wa Manchester United hasa katika kipindi hiki ambacho klabu yao inajiandaa na mchezo wake wa fainali ya kombe la Europa Ligi dhidi ya Ajax kesho Jumatano huko Friends Arena,Stockholm nchini Sweden.
Habari yenyewe ni kwamba ng'ombe mmoja maarufu sana nchini Uholanzi anayeitwa,Sijtje ametabiri kwamba Manchester United itafungwa na Ajax kwenye mchezo wao wa kesho wa fainali ya michuano ya kombe la Europa Ligi.
Ng'ombe huyo ambaye amekuwa na asilimia 85 za usahihi katika tabiri zake amekuwa akitumiwa kutabiri matokeo ya michezo mbalimbali ya soka nchini Uholanzi.
Pia hivi karibuni Sijtje alitumiwa kutabiri matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi ya Uholanzi ambapo alifanya utabiri uliokuja kuwa sahihi baada ya matokeo halisi kutangazwa.Sijtje aliwekewa ndoo 11 za chakula mbele yake na zikiwa na bendera za vyama husika ambapo ndoo ya kwanza aliyokwenda kula chakula chama chake kilishinda uchaguzi.
Mwaka 2014,Sijtje alitabiri kwamba Uholanzi ingeifunga Mexico kwenye fainali za kombe la dunia lililofanyika nchini Brazil na kweli ikawa hivyo.
Kuelekea mchezo wa kesho Jumatano Sijtje amewekewa ndoo mbili za chakula zikiwa na nembo za Ajax na Manchester United na baada ya kuachiwa kutoka kwenye banda lake alizisogelea ndoo hizo na kuanza kula kwenye ndoo yenye nembo ya Ajax kitendo ambacho kimetafsiriwa kuwa timu hiyo ya Uholanzi ndiyo itakayoibuka kidedeni.
0 comments:
Post a Comment