Paul Manjale, Dar Es Salaam.
KIPA namba moja wa Azam FC na mshindi wa tuzo ya kipa bora wa mwaka,Aishi Manula amevunja ukimya na kukanusha habari zinazoendelea kuenea kuwa yuko kwenye mipango ya kujiunga na wekundu wa Msimbazi,Simba SC.
Akitumia ukurasa wake rasmi wa Instagram,Manula amekiri kuwa mkataba wake na Azam FC uko mwishoni lakini amekanusha habari kuwa ataitosa miamba hiyo na kumwaga wino Simba SC.
Amesema "Nimekuwa nikipigiwa simu mara kwa mara na kutumiwa meseji kuwa nimesaini Simba SC.
Napenda kuwatoa hofu mashabiki wa Azam FC kuwa mimi sijasaini Simba SC.Siwezi kusaini mkataba na timu yoyote kwani mkataba wangu na Azam FC unakwenda kuisha mwezi wa 7.Kwasasa niko kwenye mazungumzo na uongozi wa Azam FC kwa ajili ya kuongeza mkataba.
Pia kisheria siruhusiwi kusaini mkataba na timu yoyote bila ya mkataba wangu wa sasa kumalizika isipokuwa naruhusiwa kusaini na Azam FC pekee kwani wao ndiyo waajiri wangu.
Naamini mazungumzo yetu yataenda vizuri na nitasaini mkataba mpya na timu iliyonitunza na kunilea mpaka leo hii.Alimaliza Manula ambaye pia ni kipa namba moja wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Manula ametoa kauli hiyo baada ya mapema wiki hii kuibuka habari kuwa yeye pamoja na nahodha wake,John Bocco Adebayor wamegomea mikataba mipya Azam FC na wako mbio kujiunga na Simba SC.
0 comments:
Post a Comment