Dar Es Salaam,Tanzania.
KAMA ilivyo desturi ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC,tayari benchi la ufundi limefanya uamuzi wa kuwapandisha vijana watano kutoka timu yake ya vijana kwa ajili ya msimu ujao 2017-18.
Vijana hao waliopandishwa ni mabeki wa kati Abbas Kapombe (aliyekuwa nahodha wa timu ya vijana), Godfrey Elias, beki wa kulia Mohamed Omary,kiungo Stanslaus Ladislaus na mshambuliaji anayekuja kwa kasi Yahaya Zaid.
Meneja wa timu hiyo, Phillip Alando,akizungumza na mtandao huu www.azamfc.co.tz amesema kuwa ujio wa wachezaji hao utazidi kuongeza orodha ya nyota waliotoka kwenye academy yao ambao wanacheza katika kikosi cha wakubwa.
“Kwa faida ya Watanzania, Azam FC imekuwa na utaratibu wa kupandisha
angalau wachezaji wawili kila msimu kutoka timu ya vijana, safari hii mwalimu (Aristica Cioaba) amekuja na majina matano, kwa hiyo uone ni kwa namna gani academy yetu inazidi kuwa bora zaidi.
“Ukiangalia kikosi cha Azam FC cha msimu ujao basi kitakuwa na wachezaji wengi sana waliotoka kwenye academy ya Azam FC,nadhani ndio timu pekee inayoongoza kuwa na wachezaji vijana wanaotoka kwenye timu zao za vijana,” alisema.
Wachezaji wengine waliopandishwa ambao wako timu kubwa ni makipa Aishi Manula, Metacha Mnata,mabeki Ismail Gambo ‘Kussi’ na Gadiel Michael, nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, Mudathir Yahya, Abdallah Masoud, mshambuliaji Shaaban Idd.
Wengine waliopandishwa ambao wako kwa mkopo ni kiungo mkabaji Bryson Raphael (Mbeya City) na Kelvin Friday (Mtibwa Sugar).
Timu kuanza mazoezi Julai 3 Katika hatua nyingine, Alando aliweka wazi kuwa kwa sasa timu ya wakubwa ipo mapumziko kwa takribani wiki tano baada ya kumalizika kwa msimu
wa ligi na kitarejea tena mazoezini Julai 3 mwaka huu, tayari kabisa kuanza maandalizi ya msimu ujao 2017/2018.
Alisema kwa sasa wapo kwenye harakati za kuifanyia kazi ripoti ya kocha wao likiwemo suala la usajili,ambapo amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia kuwa tayari wameshafanya mazungumzo na wachezaji wanaowahitaji kwa ajili ya msimu ujao.
“Kwa wachezaji ambao wanatoka nje ya Azam ambao ni wa Kitanzania,
hatuko tayari kuweka majina wazi hivi sasa, lakini kuna watu tumeshafanya nao mazungumzo, kuna watu tayari tunaelekea kumalizana nao, uongozi unajua nini unachofanya, hivyo napenda kuwaambia Watanzania usajili unaendelea chini kwa chini na hii ni vita, pale ambapo tutakuwa tumemalizana na mchezaji fulani tutaweka wazi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment