Na Faridi Miraj.
Who is Ajib? Hivi mwenyewe unajijua kama wewe ni fedha? Mimi nakuona fedha na kama mwenyewe hujioni fedha basi tatizo. Kaka yangu Saleh Kitenge shabiki wa kugalagala wa Yanga, anakupenda mno kuliko anavyompenda staa wa timu yake Donald Dombo Ngoma. Humwambii kitu kuhusu wewe. Mara nyingi nikikutana nae ananiambia nikusalimie.
Ajib unatutoa machozi dakika moja, dakika nyingine unatupa furaha. Machozi unayotutoa ni yale ya kukuona ukipapenda mno nyumbani na furaha unayotupa ni ule unyumbulikaji wako ukiwa na mpira mguuni. Tunakushangilia unavyourahisisha mpira, lakini machozi yanatoka tunavyoendelea kukuona tu.
Najisikia huzuni kila nikikutana nawe na kuanza kupiga zile stori zetu za kimjini mjini kisha tunaachana. Ndani ya nafsi naona kabisa kuna kitu sikufanyii sawa. Kwanini niendelee kukaa nawe na kuiishia kupiga stori na nisikueleze masuala ya msingi? Wacha leo nikwambie kitu mzee mwenzangu.
Rafiki yangu Ajib muda wa kufunga mkanda wa ndege na kuzurula barani ulaya umewadia na muda wenyewe ndio huu. Vipi bado hujamaliza kuwatapisha wale watu wako kwenye uwanja Taifa wanaopenda kuketi chini ya ile TV ya kuonyesha matangazo uwanjani?.
Hata kama bado jilazimishe tu uondoke. Wale wanaokushangilia wakati huu ndiyo watakao kuzomea kesho. Najua unalijua hili, labda ulete ukaidi wako wa Ilala. Sitaki kuona ukizomewa mbele yangu. Unazomewaje sasa wakati wengi tukiwa uwanjani kukutazama huwa tunakunja miguu yetu hadi nne tukiwa na uhakika na unachokifanya?
Kuzomewa kwa mchezaji wa daraja lako ni kuutusi mpira. Usisubili mashabiki wautusi mpira ndiyo uanze kutafuta safari za kwenda nje wakati ukiwa na miaka 28. Kwanini ufike kote huku?
Kuna sehemu kuna shida kwenye mpira wetu sio bure. Na shida hii ndiyo inayofanya tuendelee kumuona Ajib kwenye viunga vyetu na tusimuone kwenye viunga vya nje. Mchezaji mwenye muono wa mpira kama yeye mwenye umbo zuri na umri sahihi anaendeleaje kushangiliwa na mashabiki ambao siku akiamka vibaya ndiyo wanakuwa wa kwanza kumzomea?
Nimewahi kuzungumza na Ajib mara mbili tu kuhusu kwenda nje, lakini mara zote hana jibu la maana alilonipa zaidi tunabaki kushangaana. Mimi nalishangaa jibu lake naye analishangaa swali langu. Mshangao wetu hauna tofauti na mshangao wa Serikali unaomtafuta Faru John muda mrefu sasa bila mafanikio.
Ajib mwenyewe anajishangaa. Jinsi sisi tunavyomshangaa yeye ndiyo hata yeye anavyotushangaa sisi. Tumebaki kushangaana. Nani anayejua undani wa majaribio yake kule Misri mwishoni mwa mwaka jana? Aliwahi kuniambia hajui hata matokeo ya majaribio yenyewe.
Zamani kidogo, siku moja katikati ya mazoezi ya wachezaji wa Yanga, mwalimu wao hayati Tambwe Leya aliipanga timu yake kucheza mechi mazoezi na baada ya dakika kadhaa alipuliza kipyenga kuashiria mchezo usimame bila tatizo kutokea uwanjani. Wachezaji walimshangaa kocha wao na kumuuliza kocha vipi imekuwaje? Leya aliwakusanya wachezaji wake na kuwaambia kwa sauti ya unyenyekevu "Jamani kiukweli Said Mwamba anajua sana mpira. Kila tukija uwanjani kufanya mazoezi mara nyingi natamani mpira apewe yeye nione ufundi alionao.
Leya baada ya kumaliza maneno hayo alimalizia kwa kusema, lakini anaweza kufa masikini asipojiangalia"alimaliza Leya na kupuliza kipyenga chake kuashilia mazoezi yaendelee.
Leya hakuwa mbali na ukweli. Nilikuwa sehemu ya watu waliofika nyumbani kwa Mwamba kwa ajili ya taratibu za kumsitiri japo wakati huo sikuwa mwandishi. Andiko langu mwenyewe linanitoa machozi hapa. Nimekumbuka mengi sana. Itoshe kusema niishie hapa. Wacha stori ya kumuhusu Mwamba niikatishe tuendelee na Ajib.
Rafiki yangu Ajib nilichokiona kwa Mwamba mpaka kikanitoa machozi sitaki kikutokee na wewe. Mwamba alicheza mpira mkubwa ambao haukuwa na thamani halisi ya maisha yake. Alikuwa na maisha ya kawaida ambayo hayakuendana na hadhi ya jina lake nchini.
Unachezaje Simba, Yanga kisha hauna uhakika na kesho yako kwenye maisha? Ajib yatafakari maneno haya!
Amka usingizini, kichukie kitanda chenye mashuka mazuri na zima kiyoyozi 'AC' na anza kukimbizana na upepo kisha jiulize uliko, ulikotoka na unakokwenda. Mwanadamu timilifu ni yule anayeishi na hofu na Mungu na kujiwekea malengo. Bado hujachelewa nafasi iko.
Siku zote ujinga saa ya kwenda, saa ya kurudi hakuna ujinga. Kuna vitu unatakiwa uanze kuvichukia ndiyo ufikie waliko rafikizo Samata na Farid Mussa. Chukia zile sehemu tunazokutana wakati wa mapumziko na jipendekeze sehemu za kufanyia mazoezi magumu.
Zile nguvu za Wanyama zinazowapa shida mitoto ya kizungu hazijaja akikesha kucheza Playstation na kujifunika shuka kujikinga na baridi kali la Ulaya nyakati za Alfajiri, zilikuja baada ya kufahamu alikotoka ni kubaya zaidi kuliko aliko. Anarudi vipi Kenya wakati huu na aachane na mshahara mnono wa Wazungu? Ajib mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe.
Ubora wa Ajib hauendani na anachokifikiri kama mchezaji aliye tayari kuondoka Tanzania kwenda nje. Anatakiwa kupachukia hapa na kuondoka zake, lakini asituchukie na sisi marafikize.
Moja ya kitu kikubwa namshauri aanze programu maalum ya kuutunisha mwili. Ajib ana nishati ya kawaida isiyofanana na anavyoufanya mpira. Kuwika soka la wenzetu kuna mambo mengi zaidi ya kuuchezea mpira na kupiga pasi murua inayoweza kuusisimua uwanja mzima. Ajib unalijua hili?
Ajib arudi kwenye mazoezi ya kuongeza mwili ili aweze kujihami na mapambano ya vita kali ya watu aina ya Khalidou Koullibary kile kitasa cha Senegal na Napoli kinacholiliwa kisajiliwe na timu zote kubwa duniani hivi sasa.
Nisikudanganye mzee mwenzangu una kitu ninachokiona kwenye miguu yako na kitu hicho hajapewa kila mchezaji. Lakini swali la msingi uko tayari kukipambania kitu hicho baada ya miaka minne tuje kuzungumza mengine hapa?
Nafahamu si kazi nyepesi kwa wachezaji wetu kuondoka nyumbani haswa wakiwa kwenye vilele vya ubora wao. Eneo hili tuna zaidi ya matatizo. Matatizo yanaanzia kwa viongozi kisha inafuatia kwa wacheaji wenyewe. Shida ya viongozi ni kutaja bei kubwa kwa timu inayomtaka mchezaji. Hivi Tanzania kweli kuna mcheaji wa kuuzwa zaidi ya Sh. Milioni 80? Nenda kaulize bei za Msuva na Ndemla kisha nifuate inbox.
Shida ya wachezaji ni uoga wa kujaribu na kukutana na mazoezi magumu. Tatizo lingine ni kutenganishwa na watu wanaowapenda. Ulaya hakuna maskani wala Mkeyenge ambaye utakaa nae na mtaanza kupiga porojo. Ukitoka uwanjani kila mmoja na time yake. Mastaa wetu nyumbani hawajazoea maisha ya namna hii wamezoea kuongozana pamoja kama kundi la mbuzi.
Baada ya juzi Ajib kumpigia pasi ya outer Laudit Mavugo ambaye hakuwa na kazi nyingine zaidi ya kuweka kichwa na kufunga Samata alitokeza twitter na kuisifu pasi ile. Vipi Ajib alimuelewa Samatta kile alichokiandika au hakumuelewa tumueleweshe?
Samatta mkimya kama alivyo na muda mwingi akipenda kuinamisha kichwa chake chini amefikisha ujumbe kwa style ya kusifia pasi ile ambayo mara nyingi nashuhudia ikipigwa na Luka Modric na kumuamsha kuwa hatakiwi kuwepo alipo, anatakiwa kuwepo mbali zaidi.
Lakini Ajib mwenyewe amejiandaaje na safari hii? Hili ndiyo swali langu la mwisho kumuuliza wakati huu ambao Samatta amemsifu na kumshitua kiaina.
Mazembe ndio imemjenga Samatta kuwa hivi alivyo. Samatta alikuwa mlaini na mwenye kipaji kama Ajib, lakini kuondoka kwake nyumbani na kwenda Mazembe ndiyo kumemjenga na kumpa ujasiri wa kuipangua ngome yeyote ile ngumu. Ni kazi ya Ajib hivi sasa kuutazama upya mkataba wake na kuja na maamuzi ya kiume ambayo hayatamfanya ajutie mbeleni huku akichukua tahadhari ya kuuheshimu na muda ambao haujawahi kuwa rafiki wa mwanadamu.
0 comments:
Post a Comment