Dar Es Salaam,Tanzania.
IKICHEZA pungufu baada ya mlinzi wake wa kulia,Janvier Bokungu,kuonyeshwa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya,Simba SC imetoka nyuma na kuichapa Yanga SC mabao 2-1 katika mchezo mkali wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliochezwa jioni ya leo katika Uwanja wa Taifa,Dar Es Salaam.
Yanga SC ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza baada ya Simon Msuva kufunga kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 5 ya kipindi cha kwanza.
Mkwaju huo wa penati ulipatikana baada ya Novarty Lufunga kumwangusha Obrey Chirwa ndani ya boksi na mwamuzi Mathew Akrama kutoka Mwanza kuamuru upigwe mkwaju wa penati.Mpaka mapumziko Yanga SCwalikuwa mbele kwa bao hilo moja.
Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Joseph Omog kipindi cha pili ya kuwaingia Shiza Kichuya na Jonas Mkude yaliinufaisha Simba SC ambapo ilianza kucheza soka maridadi na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha kupitia kwa Laudit Mavugo aliyefunga kwa kichwa dakika ya 66 akimalizia krosi safi ya Shiza Kichuya kutoka wingi ya kulia.
Dakika ya 82 Shiza Kichuya aliihakikishia Simba SC ushindi baada ya kufunga bao la pili kwa mkwaju mkali wa mbali uliomshinda kipa wa Yanga,Deogratius Munish Dida na kutinga wavuni na kufanya mchezo uishe kwa Simba SC kuondoka na ushindi wa mabao hayo 2-1.
Ushindi huo umeifanya Simba SC ifikishe alama 54 baada ya kushuka dimbani mara 22.Yanga SC ni ya pili ikiwa na alama 47.
0 comments:
Post a Comment