Aliyekua mshambuliaji wa klabu ya Young
Africans pamoja na timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Sunday Manara
amewatuhumu wachezaji wa klabu hiyo kwa kusema hawakutambua umuhimu wa mchezo
wao wa jumamosi dhidi ya Simba na badala yake wakashindwa kutumia muda na
nafasi walizozipata.
Sunday Manara ambaye ni baba mzazi wa afisa
habari wa Simba Haji Manara amesema Yanga walipaswa kuwa na nidhamu ya mchezo
wakati wote kwa kucheza soka bila kuwadharau wapinzani wao, lakini walishindwa
kutimiza wajibu huo wakajikuta wakiadhibiwa na kupoteza point tatu.
Akitolea mfano kwa upande wa Simba,
mwanasoka huyo wa zamani amesema kilichowasaidia Simba ni kutovunjika moro na
kutumia ari waliyokua nayo, jambo mbalo lilikosekana kwa Young Africans ambao
walionyesha kucheza kwa mazoea.
Hata hivyo Sunday manara ambaye alibahatika
kuwa mtanzani wa kwanza kucheza soka la kulipwa barani Ulaya, amewakumbusha
baadhi ya mashabiki na wanachama wa Young Africans ambao wameanza kumnyooshea
kidole kocha George Lwandamina kwa kusema hafai, kwa kusema wakumbuke mfumo unaotumiwa
na viongozi wao kwa sasa.
Sunday amesema mfumo na mikakati ya kuwa na
wachezaji tangu wakiwa na umri mdogo ambao wanaweza kukuzwa ndani ya klabu hiyo
umeachwa hivyo kinachofanyika kwa sasa ni kuwategemea wachezaji wakigeni ambao
wanaonekana kuchoka kutokana na kutumikiswa kila siku.
Kuhusu harufu ya ubingwa ambayo inaelekezwa
Msimbazi baada ya matokeo ya mabao mawili kwa moja siku ya jumamosi, Sunday
manara amesema bado ni mapema mno kufikiria suala hilo, japo amekiri tofauti ya
point tano iliopo sasa kati ya Simba na Yanga inaweza ikawa chanzo kwa Wekundu
wa Msimbazi kujifuta machozi ya kukosa taji la Tanzania bara kwa miaka mitano
iliyopita.
0 comments:
Post a Comment