London,England.
ARSENAL imefuzu robo fainali ya michuano ya kombe la Emirates FA CUP baada ya Jumatatu usiku ikiwa ugenini kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sutton United kwenye mchezo wa raundi ya tano uliochezwa huko kwenye dimba la nyasi bandia la Borough Sports Ground,Gander Green Lane,London Kusini.
Lucas Perez alianza kuifungia Arsenal bao la kwanza katika dakika ya 26 baada ya kupokea pasi ndefu kutoka kwa Granit Xhaka kabla ya Theo Walcott kuongeza la pili katika dakika ya 55 akimalizia vyema pasi ya Alex Iwobi.
Hilo limekuwa bao la 100 kwa Walcott kufunga akiwa na Arsenal aliyojiunga nayo miaka 10 iliyopita akitokea Southampton kwa ada ya Pauni Milioni 12.
Sasa Arsenal itacheza na Lincoln City katika mchezo wa robo fainali utakaochezwa kati ya Machi 10 -13.
0 comments:
Post a Comment