Barcelona,Hispania.
Lionel Messi pichani akipongezwa na wachezaji wenzake wa Barcelona baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Leganes nyumbani Camp Nou jana Jumapili usiku.
Messi alianza kuipatia Barcelona bao la kwanza katika dakika ya 4 tu ya mchezo baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Luis Suarez aliyekuwa amegongeana vyema na Neymar.
Messi tena alikuwa shujaa wa Barcelona baada ya kupachika bao la pili kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 90.Mkwaju huo wa penati ulipatikana baada ya Neymar kufanyiwa madhambi na beki wa Leganes,Mantovani na mwamuzi kuamuru upigwe mkwaju wa penati.
Bao la kufutia machozi la wageni Leganes limefungwa na Unai Lopez katika dakika ya 71 baada ya kuunasa mpira uliomtoka mlinzi Sergi Roberto na kumfunga kirahisi kipa Marc-Andre ter Stegen.
Aidha Barcelona watapaswa kumshukuru kipa wao Marc-Andre ter Stegen baada ya kuokoa michomo miwili ya hatari iliyoelekezwa langoni mwake na Nabil El Zhar.
Mahudhurio hafifu
Kwa mara ya kwanza Barcelona imeshuhudia mahudhurio hafifu katika uwanja wake wa Camp Nou baada ya mashabiki 63,378 pekee kujitokeza katika mchezo wa Jana.Kwa kawaida Camp Nou huchukua zaidi ya mashabiki 90,000.
0 comments:
Post a Comment