Turin,Italia.
JUVENTUS imekuwa timu ya kwanza kufuzu hatua ya fainali ya michuano ya mwaka huu ya michuano ya klabu bingwa ya Ulaya baada ya Jumanne usiku kuifunga AS Monaco mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano wa hatua ya nusu fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Juventus Arena huko jijini Turin,Italia.
Mabao ya Juventus iliyokuwa inasaka rekodi ya kufuzu fainali kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu yamefungwa na beki wa kimataifa wa Brazil Dani Alves na mshambuliaji wa kimataifa wa Croatia Mario Mandzukic.Bao la kufutia machozi kwa upande wa AS Monaco limefungwa na kinda wa Ufaransa,Kylian Mbappe.
Ushindi huo umeifanya Juventus ifuzu fainali kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kushinda mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita huko Stade Loius II.
Juventus itacheza fainali na mshindi katika ya mahasimu Real Madrid au Atletico Madrid ambao leo Jumatano wanacheza nusu fainali yao ya pili.Katika nusu fainali ya kwanza Real Madrid ilishinda mabao 3-0.Fainali itachezwa June 3 huko Cardiff,Wales.
0 comments:
Post a Comment