Zurich,Uswisi.
LIONEL Messi sasa ruksa kuichezea timu yake ya taifa ya Argentina hii ni baada ya leo jioni shirikisho la vyama vya soka duniani (FIFA) kutengua adhabu yake ya kufungiwa michezo minne iliyokuwa ikimkabiri.
Mwezi Machi mwaka huu Messi alifungiwa michezo minne na kamati ya nidhamu ya FIFA akituhumiwa kumtusi mwamuzi msaidizi kwenye mchezo kuwania tiketi ya kushiriki kombe la dunia ambapo Argentina iliichapa Chile bao 1-0 lililofungwa na Messi mwenyewe kwa mkwaju wa penati.
Mbali ya kukumbwa na adhabu hiyo pia Messi mwenye umri wa miaka 29 aliamuliwa kulipa faini ya Pauni 8,100.
Taarifa iliyochapishwa leo Ijumaa kwenye mtandao wa FIFA imesema "Kamati ya rufaa ya shirikisho hilo imetengua adhabu hiyo baada ya kuridhika na rufaa iliyokatwa na chama cha soka cha Argentina pamoja na Lionel Messi mwenyewe".
Hii ina maana kwamba sasa Messi anarejea kuiongoza Argentina kusaka ushindi kwenye michezo mitatu iliyosalia ya kuwania tiketi ya kucheza kombe la dunia dhidi ya Uruguay,Venezuela na Peru.
0 comments:
Post a Comment