Dar Es Salaam,Tanzania.
DAKTARI mkuu wa mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania bara,Yanga SC,Edward Bavu leo ametoa habari njema kuhusu afya za nyota watatu wa kimataifa wa klabu hiyo Justine Zullu,Donald Ngoma na Thabani Kamusoko kuelekea mchezo wao wa Jumamosi hii wa hatua ya mtoano ya michuano ya kombe la shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria.
Akimwongelea Zullu ambaye juzi Jumamosi alichanika nyama za ugoko baada ya kuchezewa rafu mbaya na kiungo wa Azam FC,Himid Mao,Bavu amesema mchezaji huyo anayetokea Zambia kwa sasa anaendelea vizuri na matibabu na kuna uwezekano mkubwa kuwa Jumamosi ijayo akaivaa MC Alger.
"Zullu anaendelea vizuri na matibabu,asubuhi hii nilikuwa naye nikimpatia matibabu.Baada ya masaa 72 tutatoa taarifa juu ya lini ataanza mazoezi lakini kuna uwezekano kuwa akawepo uwanjani siku ya Jumamosi.Hajavunjika mfupa kama inavyoripotiwa na baadhi ya watu.
Wakati huohuo Bavu amesema wachezaji wengine wa klabu hiyo waliokuwa majeruhi Donald Ngoma na Thabani Kamusoko wao wanaendelea vizuri na tayari wameshaanza mazoezi lakini mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi,Hamis Tambwe yeye bado anasumbuliwa na maumivu ya goti na hatarajiwi kurejea uwanjani hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment