Kazan,Urusi.
HATIMAYE kiungo wa zamani wa Arsenal na Cameroon,Alex Song,amepata timu mpya baada ya leo hii kujiunga na Rubin Kazan ya Urusi akitokea Barcelona.
Song,28,ambaye jina lake kamili ni Alexandre Dimitri Song Billong,amejiunga na Rubin Kazan akiwa mchezaji huru baada ya Barcelona kumtupia virago licha ya kubakisha nae mkataba wa mwaka mmoja.
Song alijiunga na Barcelona mwaka 2012 akitokea Arsenal kwa mkataba wa miaka mitano kwa dau la £17m lakini kutokana na kuandamwa na majeruhi ya mara kwa mara hali iliyopelekea kiungo huyo kushindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha miamba hiyo ya Nou Camp.
Katika kipindi cha miaka minne alichokuwa na Barcelona,Song,alifanikiwa kucheza michezo 65 pekee,akifunga bao moja hali iliyopelekea atolewe kwa mkopo kwenda Westham United ambako nako alishindwa kufanya vizuri kama ambavyo alivyofanya katika kipindi cha miaka sita alichokuwa na Arsenal ambapo alicheza michezo 138 na kupachika mabao saba.
0 comments:
Post a Comment