SERIKALI imeliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumtumbua ofisa
wake anayehujumu uchaguzi wa Yanga kabla wao hawajamchukulia hatua
kali.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT),
Mohammed Kiganja alisema uchaguzi wa Yanga upo kama ulivyopangwa awali,
ingawa kuna baadhi ya watu wanadaiwa kufanya hila za makusudi kukwamisha
uchukuaji wa fomu kwa kushirikiana na Ofisa wa TFF.
“Uchukuaji wa fomu ulishaanza, lakini wapo watu na kwa bahati mbaya
wengine wamo ndani ya TFF na wengine wako nje wanahangaika kuhakikisha
uchukuaji fomu haufanikiwi,” alisema Kiganja na kuongeza: “Huyu mtu sisi
tunamjua, na kuna baadhi ya watu wamekwenda pale kwa lengo la kuchukua
fomu wakanyimwa kwa kigezo Jumamosi na Jumapili sio siku za kazi, bahati
mbaya zaidi hata kwenye mtandao hawakuweka mpaka tulipowakoromea jana
(juzi), ndio wameweka, “ alisema.
“TFF imchukulie hatua haraka iwezekanavyo ofisa huyo kabla sisi
hatujamchukulia hatua,” alisisitiza Kiganja na kuongeza kuwa bado
wanawasaka wengine wa nje, ambao wanashinikiza uchaguzi usifanyike. “Nia
ya serikali kuona klabu, vyama na mashirikisho yote ya michezo
wanaheshimu sheria, kanuni na katiba zilizopo.”
Kiganja, akizungumzia ombi la wazee wa Yanga la mkutano wa dharura
alisema; “ “Hakuna mkutano wa dharura waende kwenye uchaguzi, walikuwa
wapi siku zote mpaka wasubiri serikali iitishe uchaguzi ndipo watake
mkutano, walete kimaandishi na hata wakileta hatuwapi kibali.....Kama
wanampenda sana Manji wamwambie achukue fomu waende kwenye uchaguzi
wamchague kwa kura za kishindo,” alisema.
Mwishoni mwa wiki Baraza la Wazee wa Yanga, kupitia kwa Katibu wake,
Ibrahim Akilimali waliiangukia TFF na BMT kuwaruhusu wafanye mkutano wa
dharura wajadili uchaguzi wao ikiwa ni pamoja na kuwapa muongozo wa kadi
zitakazotumika kwenye uchaguzi wao.
Aidha, Kiganja aliwataka wadau wajitokeze kuchukua fomu za uongozi
ndani ya klabu hiyo na kwamba uchukuaji fomu ukiendelea kusuasua, BMT
italazimika kuvunja sekretarieti nzima ya Yanga na kuunda kamati ya
mpito itakayofanya kazi ndani ya miezi mitatu ikiandaa uchaguzi mpya.
Naye Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema huenda uchukuaji fomu
ukasogezwa mbele kwa siku mbili zaidi na kwamba Kamati ya Uchaguzi
ilitarajiwa kukaa jana jioni kuzungumzia uchaguzi huo ambao umepangwa
kufanyika Juni 25.
Uchukuaji wa fomu ulianza Mei 24, mwaka huu na kufikia jana
ilitarajiwa orodha ya wagombea ingekuwa imepatikana kabla ya kuanza kwa
taratibu nyingine kuelekea uchaguzi huo.
Ukomo wa uongozi wa Yanga chini ya Yusuf Manji ulikuwa Juni 2014,
lakini wanachama waliridhia kumuongezea mwaka mmoja kwa kile walichodai
aweze kukamilisha baadhi ya mambo ambayo alikuwa hajayakamilisha.
Hata hivyo, muda wa nyongeza huo wa mwaka mmoja ulimalizika Juni
mwaka jana, lakini ukimya juu ya uchaguzi mkuu ulitawala hadi Serikali
kupitia BMT ilipoingilia kati na Aprili 19 kuiagiza TFF ihakikishe Yanga
inafanya uchaguzi wake ndani ya siku 72.
0 comments:
Post a Comment