728x90 AdSpace

  • Latest News

    Tuesday, September 08, 2015

    MKWASA AIKOSHA TFF,YAJIPANGA KUMFANYIA MAKUBWA

    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lipo katika mchakato wa kumpa Mkataba wa kudumu, kocha wa muda wa timu ya taifa, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa.

    Pamoja na kucheza mechi tatu bila kushinda, lakini TFF imeridhishwa na maendeleo ya timu kutoka ilivyokuwa chini ya kocha Mholanzi, Mart Nooij na imeshawishika kumpa Mkataba wa kudumu Mkwasa.

    Kiwango kizuri ambacho timu ilionyesha katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Nigeria kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ndicho kimeifanya TFF ifikirie hilo.

    Aidha, TFF pia baada ya kukusanya maoni ya wachezaji mmoja na wote kuridhishwa na benchi la Ufundi la sasa la timu- inaona hakuna sababu ya kutowapa Mkataba wa kudumu Mkwasa na benchi lake.

    Washambuliaji wawili wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta pamoja na Nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga SC ya nyumbani walisema timu imebadilika chini ya Mkwasa.

    Viungo Himid Mao wa Azam FC na Said Ndemla wa Simba SC nao walisema timu imebadilika mno kutoka ilivyokuwa chini ya Nooij.
    Lakini inafahamika Mkwasa ni kocha wa Yanga SC anayefanya kazi na Mholanzi, Hans van der Pluijm na kuhusu hilo, klabu hiyo imesema haina shida kumuachia.

    Katibu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha amesema kwamba wako tayari kumuachia Mkwasa akafanye majukumu ya kitaifa.

    “Tunachoomba tu TFF wafuate utaratibu wa kuvunja mkataba, ana Mkataba na sisi wa miaka miwili, ambao ameutumikia kwa miezi minane tu,”amesema Tiboroha.

    Rais wa TFF, Jamal Malinzi alimteua Mkwasa kukaimu Ukocha Mkuu Taifa Stars kwa miezi mitatu tangu Julai na akasema kwa kuanzia atakuwa anachukua mshahara alikuwa analipwa Nooij.

    Nooij aliyekuwa analipwa dola za Kimarekani 12,500 (zaidi ya Sh. Milioni 25) kwa mwezi, alifukuzwa mwishoni mwa Juni baada ya Taifa Stars kufungwa mabao 3-0 na Uganda Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika mechi ya kufuzu CHAN.

    “Kocha Mkwasa atakua akipewa hudumu zote na masilahi (zikiwemo posho) alizokuwa anapewa kocha aliyeondoka, pia amepewa nafasi ya kuchagua benchi lake la ufundi la kufanya nalo kazi, hivyo nawaomba wadau wa mpira wa miguu na watanzania kwa ujumla tuwape sapoti makocha hao wazawa” alisema Malinzi wakati anamtangaza Mkwasa.

    Mkwasa aliwateua Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ kuwa Mshauri wa Ufundi, Hemed Morocco kuwa Kocha Msaidizi na Manyika Peter kuwa kocha wa makipa wakichukua nafasi za Salum Mayanga na Patrick Mwangata.

    Aidha, Omar Kapilima aliteuliwa kuwa Meneja na Hussein Swedi ‘Gaga’ kuwa mtunza vifaa vya timu- kukamilisha sura mpya kabisa ya benchi la Ufundi la Taifa Stars.

    Na tangu hapo timu imcheza mechi tatu bila ushindi ikitoa sare ya 1-1 na Uganda mjini Kampala kufuzu CHAN, ikifungwa 2-1 na Libya mchezo wa kirafiki mjini Kartepe, Uturuki na kutoa sare ya 0-0 na Nigeria mwishoni mwa wiki.

    Hayo yalikuwa mabadiliko makubwa kutoka kwenye timu kufungwa mechi tano mfululizo na kwa ujumla kucheza mechi 11 bila ushindi chini ya Nooij.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: MKWASA AIKOSHA TFF,YAJIPANGA KUMFANYIA MAKUBWA Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top