Kocha wa Chelsea Jose Mourinho huenda akakumbwa na adhabu ya kufungiwa michezo mitano kwa kosa la kutoa lugha ya matusi kwa daktari wa zamani wa klabu hiyo Eva Carneiro katika mchezo wa ufunguzi wa ligi kuu dhidi ya Swansea City uliochezwa hapo mwezi Agosti.
Kutoka England taarifa zinasema kitengo cha nidhamu cha FA kimeanza kuzifanyia uchunguzi picha za video ili kujiridhisha baada ya tuhuma kuibuka kuwa Mourinho alimtukana Carneiro akiwa benchi ama akirejea benchi kutoka uwanjani alikokuwa ameitwa na mwamuzi Michael Oliver kwenda kumtibu winga Eden Hazard aliyekuwa ameumia.
Chini ya kifungu cha sheria namba E3 cha FA kinasema "Wachezaji na makocha wanaweza kuadhibiwa kwa adhabu isiyopungua michezo mitano kwa kosa la kutumia lugha za matusi na ishara zisizofaa wawapo viwanjani.
Tukio hilo linakuwa la pili kwa Mourinho ambaye msimu uliopita aliingia tena matatani na kulimwa faini ya £25,000 na FA baada ya kudai kuwa kuna mchezo mchafu uliokuwa ukifanywa ili kuhakikisha Chelsea haitwai ubingwa wa ligi kuu.Mourinho aliyatoa madai hayo baada ya kiungo wake Cesc Fabregas kunyimwa penati na mwamuzi Anthony Taylor katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Southampton.
0 comments:
Post a Comment