KLABU ya Simba SC itaanza kuwapa tuzo wachezaji wake kila mwezi, ili kuongeza morali katika kikosi cha timu hiyo kinachoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva amesema kwamba tuzo ya kwanza itatolewa mwishoni mwa mwezi huu.
Aveva amesema kwamba uongozi umeamua kufanya hivyo ili kuunga mkono juhudi za wanachama na wapenzi wa Simba wanaothamini mno mchango wa wachezaji katika kuifanya timu.
"Hivyo tumeona ni jambo la busara kuwa klabu ya kwanza Tanzania kuwa na tuzo za Mchezaji wake bora. Tunaamini kwamba tuzo ya Mchezaji bora wa mwezi wa Simba itaongeza ari na kujituma kwa wachezaji wetu.
Sisi tukiwa kama viongozi ni kazi yetu ya msingi kuhakikisha kuwa wachezaji wetu hasa wale wanaojituma zaidi wanatambuliwa na kuenziwa,"amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya EAG Group ambao ni washauri na watekelezaji wa Masoko na Biashara wa Simba SC, Imani Kajula ameelezea namna mchakato huo utakavyokuwa ukifanywa.
"Wanachama na wapenzi wa Simba na wapenda michezo ndio watakao kuwa wanachagua mchezaji bora wa mwezi kwa kutuma jina la mchezaji wanayempendekeza kwenda kwenye namba 15460, Ni wale tu ambao wamejiunga na Simba News kupitia mtandao wa Voda na Tigo wataweza kupiga kura kuchagua mchezaji bora wa mwezi wa Simba,"amesema.
Kwa mwezi huu, mshambuliaji Mganda Hamisi Friday Kiiza yuko katika nafasi nzuri ya kushinda tuzo hiyo, kutokana na kufunga mabao matano katika mechi tatu za mwanzo za Ligi Kuu, ikiwemo hat trick katika ushindi wa 3-1 mchezo uliopita.
Simba SC itashuka tena dimbani kesho kucheza mechi ya mwisho, itakapomenyana na mahasimu, Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Bin Zubery
0 comments:
Post a Comment