728x90 AdSpace

  • Latest News

    Tuesday, September 08, 2015

    SIMBA,YANGA NA AZAM ZAIVIMBIA TFF KUHUSU NYOTA WA KIGENI

    Dar es salaam,Tanzania

    Ingekuwa siasa tungesema Simba, Yanga na Azam zimeibuka na kuliandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga agizo la kiasi cha dola 4,000 (Sh mil 8) kama malipo ya kila mchezaji wa kigeni msimu huu.

    Rais wa TFF, Jamal Malinzi wiki kadhaa zilizopita alitoa rai hilo kwa kila klabu yenye mchezaji wa kimataifa kuhakikisha analipiwa kiasi hicho kwa ajili ya kuchangia mfuko wa maendeleo ya soka la vijana, vinginevyo hawataruhusiwa kushiriki ligi kuu.

    Kwa nyakati tofauti, viongozi wa Simba na Yanga wamesema kuwa hawapo tayari kutoa kiasi hicho kwani ni mpango wa TFF kutaka ‘kuwachuna’.

    Katibu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha alisema kwa pamoja (Simba na Azam) wameiandikia barua TFF kuomba kusitisha mpango huo mpaka pale watakapotoa tamko.

    Straika wa Yanga, Donald Ngoma, ni mmoja wa wachezaji wa kigeni walioingia kwenye ligi kuu msimu huu na kukutana na kanuni hiyo mpya.

    “Sisi (Yanga), Simba na Azam tumewaandikia barua TFF kuomba mpango huo usitishwe kwanza ili tuketi chini kulijadili, kisha tutatoa tamko la pamoja kama klabu.
    “Kwanza hakuna aliye tayari kuzilipa. Ni kiasi kikubwa, lakini jingine ni mpango wa kutukamua tu hela. Badala ya wao wawekeze kwetu (klabu), leo hii wanatutegemea sisi,” alihoji mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu Dar (UDSM).

    Simba kupitia kwa kaimu katibu mkuu, Frisch Collins, ilisema: “Kwa sasa hatuna jibu mpaka kamati itakapokaa, kisha tutalitoa ufafanuzi.”

    Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa alipoulizwa kuhusu mpango huo, alisema Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, ndiyo itakuwa na jibu la mwisho wakati wa kupitisha majina ya wachezaji wanaofaa kucheza ligi kuu msimu huu.
    “Sina jibu la moja kwa moja, tusubiri kamati hiyo ifanye kazi yake, mwisho wa yote ndiyo watatoa majina ya wachezaji wanaostahili kucheza msimu ujao, kwa hiyo tusubiri jibu litapatikana tu,” alisema Mwesigwa.

    Mgawanyo wa fedha hizo ni kwamba dola 2,000 ni kwa ajili ya leseni ya mchezaji husika huku dola 2,000 nyingine ni kwa ajili ya usajili (registration), kitu ambacho timu zimepinga vikali.

    Kwa mpango huo inamaana Yanga, Simba na Azam zenye jumla ya wageni 21, zitatakiwa kulipa zaidi ya Sh mil 160 huku timu za Mbeya City, Stand na Coastal Union nazo zikikumbana na athari ya agizo la Malinzi.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: SIMBA,YANGA NA AZAM ZAIVIMBIA TFF KUHUSU NYOTA WA KIGENI Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top