Dar es salaam,Tanzania.
KLABU ya soka ya Yanga imemtimua kipa wake namba mbili Juma Kaseja,kutokana na kushindwa kuhudhuria mazoezi ya timu hiyo tangu kuanza maandalizi ya mzunguko wa nane.
Mkurugenzi wa Habari wa klabu hiyo Jerry Muro alisema kutoka Zanzibar jana,uongozi wa Yanga umefikia maamuzi hayo baada ya kutoridhia na tabia ya utoro ya kipa huyo mkongwe nchini.
“Tumeamua kuachana na Kaseja, kiroho safi baada ya kuona anavunja makubaliano kwa kushindwa kuhudhuria kazini, cha kufurahisha ni kwamba haidai Yanga na fedha zake alishalipwa’’,alisema Muro.
Muro alisema wamefikia maamuzi hayo ili kutoa fundisho kwa wachezaji wengine wenye tabia kama hiyo ili kuimarisha
nidhamu ya timu iweze kuwa juu na kufanya vizuri katika michuano mbalimbali wanayoshiriki.
“Aliamua kususa kuja kazini bila sababu za msingi jambo ambalo lilivunja mkataba wake na Yanga na sisi baada ya kuona hatudai, tumeona ni vyema kumuachia aende anakotaka na tunamtakia kila la kheri,” alisema Muro.
Awali kipa huyo aligoma kujiunga na wenzake akidai mpaka amaliziwe fedha zake za usajili Shilingi milioni 20 na baada ya fedha Kaseja, aliandika barua kuwajulisha Yanga amepokea fedha zake na alikuwa tayari kurudi kazini, lakini uongozi wa Yanga haukumjibu.
Baada ya kuona hajibiwi, Kaseja aliamua kwenda mazoezini lakini aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mbrazil Marcio Maximo alimkataza kufanya mazoezi na kumtaka awasiliane na uongozi wa timu hiyo kwanza lakini kipa huyo hakufanya hivyo.
Moja ya sababu kubwa zilizosababisha Kaseja kushindwa kudumu na Yanga ni kuwekwa benchi na nyingine ni kudai kwamba haaminiwi na mashabiki pamoja na baadhi ya viongozi wa timu hiyo.
Kaseja alijiunga na kikosi cha Yanga kwenye dirisha dogo msimu uliopita akiwa mchezaji huru baada ya kutemwa na Simba na ameidakia timu hiyo mechi 15 nyingine akiwa benchi na kumuacha Deogratius Munish ‘Dida’ akidaka.
0 comments:
Post a Comment