Madrid,Hispania.
MRENO Cristiano Ronaldo usiku wa kuamkia leo ameifungia klabu yake ya Real Madrid mabao matatu ( hat-trick) dhidi ya wapinzani wao wa jadi Atletico Madrid kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya nusu fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya uliochezwa huko Santiago Bernabeu, jijini Madrid.
Mabao hayo matatu mbali ya kuwa karibu kuipeleka Real Madrid kwenye fainali itakayofanyika huko Cardiff, Wales baadae mwezi huu bali pia yamemfanya Ronaldo,31,aweke rekodi kubwa tano binafsi.
Kwanza yamemfanya Ronaldo afikishe mabao 103 kwenye michuano hiyo.Mabao matatu zaidi ya timu nzima ya Atletico Madrid ambayo imefunga mabao 100 pekee katika historia ya ushiriki wake kwenye michuano hiyo yenye utajiri mkubwa wa fedha.
Pili mabao hayo matatu yamemfanya Ronaldo awe amefunga hat-trick saba kwenye historia ya michuano hiyo na hatimaye kumfikia mpinzani wake wa karibu staa wa Barcelona,Lionel Messi aliyefikisha idadi hiyo miezi michache iliyopita.
Pia Ronaldo amekuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 20 katika mchezo wa wapinzani wa jadi wa jiji la Madrid yaani Madrid dabi.
Mabao hayo matatu pia yamemfanya Ronaldo awe mchezaji wa kwanza kufunga hat-tricks (mabao matatu) zimazofuatana ( back-to-back) katika hatua ya mtoano ya michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya.Ikumbukwe katika hatua ya robo fainali Ronaldo alifunga hat-trick dhidi ya Bayern Munich.
Mwisho mabao hayo matatu yamemfanya Ronaldo afikishe mabao 13 kwenye michezo ya hatua ya nusu fainali na kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye hatua hiyo.Mabao mawili zaidi mbele ya gwiji wa zamani wa Real Madrid,Alfredo Di Stefano aliyefunga mabao 11.
0 comments:
Post a Comment