Pichani wachezaji wa Barcelona B wakiwafariji wenzao wa Eldense
Paul Manjale
UNAWEZA usiamini hiki unachokisoma hapa lakini ukweli unabaki pale pale kuwa klabu ya Eldense imetangaza kujitoa kushiriki ligi daraja la tatu nchini Hispania ikiwa ni siku moja tu imepita tangu ikung'utwe mabao 12-0 na Barcelona B juzi Jumamosi.
Eldense iliyoanzishwa mwaka 1921 huko Elda,Valencia mashariki mwa nchi ya Hispania pia imetangaza kusitisha shughuli zake zote za kimichezo pamoja na kuvunja mikataba na wadhamini wao kutoka nchini Italia.
Kichapo cha mabao 12-0 ilichokipata Eldense Jumamosi kimekuwa ni cha pili kushuhudiwa kwenye ligi hiyo.Kichapo cha kwanza kilishuhudiwa mwaka 1993 pale Extremadura ilipoifunga Portuense kwa idadi kama hiyo ya mabao.
Kabla ya kujitoa huko Eldense ilikuwa imebakiza michezo sita kwenye ligi hiyo itakayofikia tamati hivi karibuni na kichapo kutoka kwa Barcelona B kilikuwa tayari kimewapa tiketi ya kushuka daraja na kwenda ligi daraja la nne.
Mpaka sasa hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kutoka ndani ya chama cha soka cha Hispania juu ya uwamuzi huo wa kujitoa kwa Eldense.
Wakati huohuo taarifa kutoka nchini Hispania zinasema uongozi wa Eldense umelitaka jeshi la polisi la Elda kufanya uchunguzi ili kubaini kama kulikuwa na hujuma zozote zile za upangaji wa matokeo kwenye mchezo huo.
0 comments:
Post a Comment