728x90 AdSpace

  • Latest News

    Wednesday, August 10, 2016

    POGA KARIBU ILA KUMBUKA “APEWAYE VINGI HUDAIWA VINGI.....


    Na Chikoti Cico.

    “APEWAYE VINGI HUDAIWA VINGI” Ni maneno manne tu lakini yenye maana kubwa sana katika maisha ya kila siku ya mwanadamu, ni maneno ambayo humfanya Mwanadamu yeyote apate kufikiria kwa makini kabla ya kufanya jambo lolote na pia hutoa motisha katika kukamilisha lengo fulani.

    Ni saa 10 jioni katika viunga vya mji wa Roissy-en-Brie nchini Ufaransa, watoto mbalimbali wenye umri wa kati ya miaka 7-12 wako nje wakicheza mpira wengi wao wakiupiga mpira kugonga ukuta, ukuta uliopambwa kwa picha ya mchezaji maarufu ambaye wengi wao wanatamani kufika alikofika.

    Kuta hizi za makazi haya ya Renardiere zimepambwa kwa picha ya Paul Pogba, picha hizi zikiakisi umaarufu wa mchezaji huyo kwenye makazi haya na pia ni picha ya “role model” wa watoto wengi wanaokuliwa katika makazi ya Renardiere ambao wanatamani kufika mbali kisoka. Renardiere ndiko mahali ambako Pogba alikulia na kucheza soka la utotoni.

    Renardiere ndiko mahali Paul Pogba akiwa na miaka miwili na nusu Baba yake na Mama yake walitengana na kumwacha kiungo huyo akilelewa kwa muda mrefu na mama yake (Yeo Moriba ) ambaye kwa muda wote amekuwa bega kwa bega na mwanae mpaka hapo alikofikia akiwa na miaka 23 sasa.

    Katika umri wa miaka 23 Paul Pogba amesaini kandarasi ya miaka minne kuichezea klabu ya Manchester United kwa rekodi ya dunia ya pauni milioni 100 akitokea Juventus alikouzwa na United kwa fidia ya pauni laki nane mwaka 2012. Kandarasi hiyo inaweza kongezeka na kufika miaka sita.

    Ukiachilia mbali rekodi hiyo ya mauzo pamoja na kandarasi aliyosaini, Pogba ataweka kibindoni mshahara wa pauni 290,000 kwa wiki, mshahara utakaomfanya kuwa mchezaji anayelipwa ghali zaidi kwenye ligi ya primia huku akipokea mshahara mnono kuliko Wayne Rooney na Zlatan Ibrahimovic ndani ya klabu ya Manchester. 

    Na kutokana na malipo ya uhamisho na mshahara atakaopokea hapo ndipo Pogba anapotakiwa kufahamu kwamba “APEWAYE VINGI HUDAIWA VINGI” mashabiki wa United watakuwa na matarajio makubwa juu ya kiungo huyo na kila mmoja ambaye ana unasaba na klabu ya Manchester atatamani kuona Pogba anarejesha mshahara na ada ya uhamisho kwa kuonyesha kandanda safi uwanjani.

    Wachambuzi mbalimbali wa soka duniani na wengine wakiwa ni wachezaji wa zamani wa Manchester wameshaanza kuonesha wasiwasi dhidi ya bei na mshahara wa Pogba na hivyo hata hawa “WATADAI” mengi kutoka kwa Pogba kwa msimu wa ligi ya primia 2016/17 .

    Ukiachana na mashabiki wa United na washirika mbalimbali wa klabu hiyo pia dunia ya soka kwa ujumla wake itamdai Pogba, kama ambayo Bale, Ronaldo, Kaka na Zidane walivyodaiwa baada ya uhamisho wao kuvunja rekodi, dunia ya soka itatamani kumwona kiungo mahiri mwenye hadhi ya pauni milioni 100 na sio vinginevyo.

    Pogba maarufu kama 'La Pioche' ama “sururu” kwa kiswahili analo jukumu zito zaidi katika kuirejesha Manchester United kwenye makali yake, kuirejesha United kwenye hadhi yake, kuirejesha United kuwa moja ya timu zinaogopwa ndani ya ligi ya primia na barani Ulaya kwa ujumla.

    Kwa mshahara wa pauni 290,000 ambao kama Pogba atakaa kwa miaka sita ya mkataba wake ndani ya United ataweka kibindoni pauni milioni 90, ni mshahara ambao utamchukua Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May miaka 629 kuweza kuwa nao na hapo ndipo unaona ni kwa jinsi gani Pogba anahitajika kuwapa “VINGI “ Manchester United kwasababu yeye pia atapokea “VINGI” kutoka kwao.

    Wakati jua linazama katika makazi ya Renardiere ndoto za watoto wengi ni kutaka kufika alikofika Pogba na wakati jua linachomoza jijini Manchester mashabiki wa United watatamani kuona ndoto zao za Manchester United ya makombe mbalimbali kila msimu zikitimizwa na Pogba na sio vinginevyo.

    Paul Pogba Karibu Manchester United, Karibu Carrington na Karibu Old Trafford.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: POGA KARIBU ILA KUMBUKA “APEWAYE VINGI HUDAIWA VINGI..... Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top