Dar Es Salaam,Tanzania.
HATIMAYE klabu ya Yanga imewasilisha rasmi barua ya utetezi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao utapelekwa kwa Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA), juu ya kushindwa kuwasilisha kwa muda majina ya wachezaji wake watakaowatumia msimu ujao.
Yanga na Coastal Union ya jijini Tanga ndizo timu zilizoshindwa kuwasilisha kwa muda majina hayo ambapo asubuhi ya jana Wanajangwani hao wamewasilisha utetezi wao kama walivyofanya pia Coastal Union.
Kwa kawaida usajili huo lazima uingizwe kwenye Mtandao wa Usajili wa Kimataifa (TMS) ambao huwa kumbukumbu hizo hutunzwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit,amesema kuwa kuwa tayari wamewasilisha utetezi huo na kudai kuwa hawakuchelewa kutuma majina hayo na badala yake mtandao ndio uliokuwa bize.
“Sisi tulipeleka majina mapema tena kwa wakati sasa tunahisi huu mtandao haukuweza kuruhusu vema usajili wetu ndio maana umeonyesha kuwa hatujawasilisha,”alisema.
Alisema uongozi wao upo makini sana katika masuala yanayoihusu timu yao na kuwatoa wasiwasi mashabiki wao kuwa timu yao haitashushwa daraja kama inavyosemekana mitaani.
“Huwa tupo makini sana na masuala hayo,nadhani kilichotokea ndicho hicho nilichokieleza hivyo mashabiki wetu wasiwn na wasiwasi wowote, naamini jambo hili litamalizika vizuri tu,” alisema.
Kwa mujibu wa kanuni za FIFA, klabu inayochelewesha kutuma majina ya wachezaji itakaowatumia inatakiwa kutoa utetezi unaojitosheleza na endapo ukikataliwa timu husika hushuka daraja ambalo halimo kwenye usajili wa mfumo wa TMS.
Juzi TFF ilizitaka timu zilizoshindwa kuwasilisha majina hayo kuwasilisha barua za utetezi, ili nao wazitume FIFA na kusubiri majibu kama utetezi huo utakubalika ama la.
0 comments:
Post a Comment