Dar es Salaam,Tanzania.
SIKU tatu baada ya kukabidhiwa mikoba ya kuwa Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Joseph Omog amewataka viongozi wake kumfuatilia mshambuliaji Didier Kavumbagu ili kuona kama kuna uwezekano wa kufanya naye kazi msimu ujao.
Kavumbagu amemaliza mkataba wa kuitumikia Azam FC mwishoni mwa
msimu uliopita na ni mmoja wa wachezaji wa kimataifa waliokataa kuendelea kuitumikia timu hiyo msimu ujao kutokana na kuwa na msimu mbaya kwa kusota benchi chini ya kocha Stewart Hall.
Omog, amesema anamhitaji Kavumbagu, aweze kufanya naye kazi kwa sababu ni mshambuliaji anayeujua vizuri uwezo wake anapokuwa uwanjani.
“Kavumbagu ni mchezaji mzuri nimefanya naye kazi Azam alikuwa mshambuliaji wangu tegemezi,ukiacha John Bocco na Kipre Tchetche na aliweza kuongoza kwa ufungaji nimeutaka uongozi kuangalia kama kuna uwezekano wa kumpata maana nimesikia amemaliza mkataba na Azam,” alisema Omog.
Kocha huyo raia wa Cameroon alisema kuwa na Kavumbagu kwenye
safu ya ushambuliaji ni faida kubwa kwani ni mchezaji anayejua vizuri majukumu yake na anajua kitu gani anatakiwa kuifanyia timu yake ili iweze kufaidika na yeye.
Aidha kocha huyo alisema mbali na kumhitaji Kavumbagu pia ataongeza washambuliaji wengine kutoka nje ambao watashirikiana na wale waliopo Ibrahim Ajibu na Danny Lyanga, mikakati yake ikiwa ni kuwa na safu kali ya ushambuliaji itakayompa uhakika wa ushindi katika kila mchezo watakaocheza.
“Huwezi kuwaza ubingwa kama huna safu ya ushambuliaji kali ambayo inakupa uhakika wa mabao mawili hadi matatu, katika kila mchezo ndiyo maana nataka kuimarisha safu ya ushambuliaji baada ya hapo nitakuja kwenye ulinzi na kumalizia eneo la kiungo,” alisema Omog.
Usajili wa kwanza kwa kocha Omog,anatarajiwa kuwa mshambuliaji
D’abidian Blagnon raia wa Ivory Coast ambaye tayari amewasili nchini usiku wa kuamkia jana na alitarajiwa kuanza majaribio yake jana jioni kama kiwango chake kitamvutia Mcameroon huyo atapewa mkataba.
0 comments:
Post a Comment