Zanzibar,Tanzania
KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC,Zeben Hernandez, ameendelea kukiandaa kikosi chake kisayansi zaidi,ambapo leo amewashangaza baadhi ya wakazi wa Visiwani Zanzibar baada ya kuwafanyisha zoezi la kuendesha baiskeli barabarani wachezaji wake.
Kikosi cha Azam FC hivi sasa kinaendelea na mazoezi makali visiwani hapa ilipoweka kambi ya wiki moja, ambapo katika muendelezo wa mechi za kirafiki jana iliweza kuichapa Kombaini ya Wilaya ya Mjini bao 1-0,lililofungwa na mshambuliaji aliyeko
kwenye majaribio Fuadi Ndayisenga.
Katika muendelezo wa programu zake kwenye kambi hiyo, leo saa 4 asubuhi Zeben aliwafanyisha zoezi la kuendesha baiskeli wachezaji wake,wakiendesha kwa takribani saa mbili wakianzia katika Hoteli ya Mtoni Marine walipofikia kuelekea Bububu hadi Amaan na kuitafuta tena njia ya kurejea hotelini walipoanzia.
Programu hiyo mpya kabisa kwa wachezaji ambayo haijazoeleka kufanywa na wachezaji wa timu yoyote
hapa nchini, ilisimamiwa kwa ukaribu na Kocha Msaidizi wa Viungo wa Azam FC, Pablo Borges.
Licha ya ugumu wa programu hiyo ya kuendesha baiskeli umbali mrefu pamoja na kupanda vilima vitatu tofauti pamoja na mvua iliyokuwa ikinyesha kwa nyakati tofauti,wachezaji walionekana kufurahia mazoezi hayo, ambayo ni mahususi kwa kujenga nguvu za miguu, pumzi na kasi.
Cha kufurahisha zaidi kila eneo walilopita watu walionekana kushangaa wakidhania ni mashindano ya baiskeli, lakini baadaye walikuja kugundua ni mazoezi tu ya wachezaji wa Azam FC na kubakia kuwashangilia na kuwapungia mikono kila walipopita.
Mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz ulifanya mahojiano maalumu na Kocha Zeben, ambaye alieleza kufurahishwa na zoezi hilo na kudai kuwa mazoezi hayo ni muhimu kwa wachezaji wake katika kipindi hiki wanapojiandaa na msimu ujao.
“Kiukweli haya ni mazoezi ya kwanza ya kuendesha baiskeli, nimefurahia sana kwa namna tulivyofanya,lakini wachezaji wote nao wanaonekana wanafuraha, lengo la kuja Zanzibar si tu kuja kufanya mazoezi uwanjani,tumekuja huku kutengeneza timu wachezaji wote waweze kuelewana kila mmoja na kufanya vitu kwa pamoja.
“Tunamshukuru Mungu tumekwenda na kurudi salama, hivyo kwa sasa tumekuja kupumzika kidogo kabla ya kwenda kufanya mazoezi mengine uwanjani baadaye,” alisema Zeben.
Anaionaje kambi ya Zanzibar Akizungumzia kambi ya Zanzibar wanayoendelea nayo kwa siku ya nne leo, Zeben alisema kuwa wameipokea vizuri kambi hiyo huku akieleza kufurahishwa na wachezaji wote pamoja na msafara mzima wa Azam FC uliokuwa visiwani hapa.
“Tumefurahishwa sana na kambi ya hapa hata program ya mazoezi tunayoendelea nayo, malengo yote tuliyoyapanga kwenye kami hii ya hapa yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa,kwa sasa tunaangalia ni programu gani zilizobakia ili tuweze kufanya vizuri msimu ujao, lakini mpaka sasa mazoezi yanakwenda vizuri pamoja na kazi zote tulizozifanya,” alisema.
0 comments:
Post a Comment