Dar es Salaam,Tanzania.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imelipandisha kizimbani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushindwa kumlipa Mkurugenzi wa Kampuni za usambazaji wa vifaa vya michezo Smart Sports General na Dar Solution General Supplies, George Wakuganda, kiasi cha Sh milioni 17.7.
Kesi hiyo namba 175 ya mwaka 2016,ilifunguliwa Juni 27 mwaka huu, mahakamani hapo lakini ilishindwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Magreth Bankika, kutokana na upande wa TFF kutofika mahakamani.
Hata hivyo, Wakili wa mdai, Iren Mahila,alidai mahakamani hapo kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa lakini upande wa TFF umeshindwa kufika mahakamani licha ya kupewa taarifa.
Kutokana na sababu hiyo, Hakimu Bankika alisema hawezi kuendelea kusikiliza shauri hilo hadi upande wa TFF utakapofika mahakamani hapo.
Hakimu Bankika aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 3, mwaka huu.
Awali, Wakuganda alifungua kesi ya madai dhidi ya TFF baada ya kusambaza vifaa vya
michezo ikiwemo mipira na jezi katika timu ya taifa ya wanaume, wanawake na vijana kati ya Juni 2014 hadi Machi mwaka huu lakini walishindwa kumlipa.
Alidai kuwa katika usambazaji wa vifaa
hivyo, mlalamikaji huyo alipewa hundi ya usambazaji wa vifaa kwa awamu mbili, huku ya kwanza akipewa Februari 23, mwaka huu ikiwa na thamani ya Sh milioni tisa.
Alidai kuwa mara baada ya kupewa hundi hiyo, alikwenda kutoa katika Benki ya NMB tawi la Ilala, lakini ilikataliwa akiambiwa akaunti haikuwa na kitu.
Alidai kuwa alipewa hundi ya pili Machi 29,mwaka huu ikiwa na thamani ya Sh 6, 670,000 ambapo alikwenda kutoa katika benki hiyo ya NMB tawi la Mandela Road, ambapo ilikataliwa.
Kutokana na hundi hizo kukataliwa,Wakuganda aliwaandikia barua TFF kupitia Kampuni ya uwakili ya CyberSpace Law Advocate, lakini hawakumjibu wala kumlipa
hadi alipoamua kufungua kesi hiyo Juni 27,mwaka huu.
CHANZO:BINGWA
0 comments:
Post a Comment