Siku chache baada ya kikosi cha Yanga kutupwa nje ya michuano ya
Kombe la Kagame, iliyofikia tamati jana Jumapili huku benchi la ufundi la timu
hiyo likigundua kilichoimaliza, sasa limeutaka uongozi wa klabu hiyo
kuhakikisha unamsajili kiungo mkabaji wa FC Platinum ya Zimbabwe, Thabani
Kamusoko.
Benchi hilo la ufundi la Yanga linaloongozwa na Mholanzi, Hans van
Der Pluijm, linadaiwa kufikia uamuzi huo hivi karibuni baada ya kukaa pamoja na
uongozi wa klabu hiyo na kujadili majina matatu ya viungo wakabaji waliokuwa
wamependekezwa.
Majina mengine yaliokuwa yamependekezwa na benchi hilo la ufundi
la Yanga ni pamoja na Khalid Aucho wa Gor Mahia ya Kenya pamoja na Mkenya
Anthon Akumu ambaye anaitumikia Al Khartoum ya Sudan.
Hata hivyo, miongoni mwa wachezaji hao, Kamusoko ndiye anadaiwa
kupewa nafasi kubwa ya kujiunga na timu hiyo kutokana na kupigiwa upatu na
viongozi wengi wa klabu hiyo, wakiwemo pia baadhi ya wachezeji waandamizi wa
kikosi hicho cha Yanga.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa, tayari
uongozi umeshaanza harakati za kuhakikisha unainasa saini ya kiungo huyo maarufu
kwa jina la Rasta ambaye alikuwa ni miongoni wa wachezaji wa FC Platinum
waliowasumbua vilivyo wachezaji wa timu hiyo yenye makao makuu Jangwani jijini
Dar, zilipokutana katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Endapo itashindikana kumsajili mchezaji huyo, ndipo
tutakapowageukia hao wengine lakini kwa sasa Rasta huyo ndiye chaguo letu la
kwanza.
“Kila mtu anaujua uwezo wake kwani alitusumbua sana tulipocheza na
FC Platinum, hivyo baada ya benchi letu la ufundi kugundua upungufu katika
michuano ya Kombe la Kagame kwenye nafasi ya kiungo mkabaji, likapendekeza
asajiliwe kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kuiunganisha timu, hivyo tukimpata ni matumaini
yetu kuwa atasaidiana vizuri na Makapu (Said Makapu),” kilisema chanzo cha
habari.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha ili aweze kuthibitisha juu ya taarifa hizo, hakuweza kupatikana hadi tunakwenda mitamboni, kufuatia simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa, hata hivyo kwa upande wake, mkuu wa kitengo cha habari cha klabu hiyo, Jerry Muro, alipoulizwa kuhusiana na mpango huo, alisema: “Habari hizo ni ngeni kwangu, hivyo siwezi kuzizungumzia, hivyo kama zipo basi tutawajulisha.”
0 comments:
Post a Comment