Makala na Paul Manjale.
Ukiona ndugu wanagombana wewe chukua jembe ukalime.Huu ni msemo mdogo sana wa kiswahili lakini wenye maana kubwa sana kwa aijuaye maana hiyo.Tuishie hapo,twende Catalunya.
Moja kati ya jambo ambalo silioni likitokea mapema katika dunia ya sasa ya soka ni kumuona Messi akihama Barcelona na kutua klabu nyingine.
Achilia mbali Chelsea na Psg zinazofuatilia kwa karibu mgogoro uliopo kati yake na kocha Luis Enrique.
Siseme hivi kwa kuwa sipendi kuona Messi akicheza na Eden Hazard pale Stamford blidge ama Lucas Moura pale Parc des Princes la hasha bali ni ugumu ninaouona katika kukamilika kwa ndoto hiyo.
Barcelona ni wachungu sana linapokuja suala la kuuza mchezaji wao hasa mchezaji ambaye ni kipenzi tena aina ya Messi.
Urahisi iliyoupata Chelsea kumpata Cesc Fabregas ama Arsenal kumpata Alexis Sanchez hautokuwa
sawa mara elfu na uchawi wa manoti ya Roman Abromovic katika kuipata saini ya Messi.
Barcelona ni wajanja na jeuri sana na sidhani kama wako tayari tena kurudia makosa kama waliyofanya kwa kumuuza Luis Figo kipindi kile.Wanajua kuwa mashabiki wao ni wakorofi kuliko Al shabab,paundi milioni 200 za Chelsea zitawatoa roho.
Barcelona siyo Arsenal.Wameshatamka mara nyingi kuwa wao siyo duka la kuuza wachezaji.Ukiona wameuza mchezaji ujue kwamba mchezaji huyo hahitajiki tena katika kikosi chao.
Kwa akili ya kawaida tu tena ya kuvukia barabara,je,ni kweli Messi anaelekea huko?Jibu ni hapana Barcelona bado inamuhitaji Messi pengine kuliko Messi anavyoihitaji Barcelona.
Messi amekuwa ni shamba la Barcelona nje na ndani ya uwanja.Ndani ya uwanja katika misimu 11 aliyoichezea miamba hiyo ya Catalunya Messi amesaidia upatikanaji wa mataji zaidi ya 21.Nje ya uwanja Barcelona imeendelea kuwa klabu kubwa na tajiri dunia kutokana tu na kuwa na mchezaji aina ya Messi.
Makampuni mengi ya ndani na nje ya ulaya yameingia mikataba mikubwa na minono na Barcelona kisa Messi.Unadhani wakatalunya wameshiba noti tayari hata wamuachie Messi kirahisi namna hiyo kisa hana mahusiano mazuri na Luis Enrique?Sahau!!Enrique ataondoka,Messi atabaki na sinema itakuwa imeishia hapo.
Kuondoka kwa Enrique kamwe hakutoiuma Barcelona kama itakavyokuwa katika kuondoka kwa Messi.Messi ni irreplaceable wakati Enrique ni replaceable.
Hiyo tisa,kumi alichoifanyia Messi Barcelona katika miaka 11 ya uwepo wake Camp Nou,Enrique na kizazi chake hawawezi kukifanya hata kwa miaka mia moja ijayo.
Kumuuza Messi ni sawa na kuuza moyo kisha ukategemea kuishi maisha marefu.Barcelona ya sasa siyo ile tuliyoizoea.Xavi huyu siyo yule wa pasi nyingi kama mchanga wa bahari.Iniesta nae uzee umemuita hakimbii tena kwa kazi ile ile.Messi ndiyo tegemeo pekee lililobaki,Neymar utoto mwingi,Suarez bado anauzoea mji.
Kumuuza Messi kutamaanisha kujirejesha tena utumwani Santiago Bernabeu.Kuzirejea tena zile zama za njaa na kiu kali ya mataji.Barcelona siyo Arsenal,bila mataji pale mambo hayaendi.
Kama Barcelona iliweza kumuondoka Ronaldinho, Ibrahimovic na kisha Pep Guardiola ili kuulinda ufalme wa Messi hivyo sioni ugumu kwa Jose Maria Batromeu kumuondoa Enrique ili Messi awe na furaha tena.
0 comments:
Post a Comment