KIUNGO mkabaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Justice Majabvi amewasili alfajiri ya leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kwa ajili ya kujiunga na Simba SC.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, anayetokea klabu ya Vicem Hai Phong F.C. ya Vietnam, baada ya kutua Dar es Salaam amepandishwa boti moja kwa moja kupelekwa Zanzibar, ambako kikosi cha Simba SC kimeweka kambi.
Majabvi atakuwa na siku tatu za kutazamwa na kocha Muingereza Dylan Kerr kabla ya usajili wake kuidhinishwa.
Kiungo huyo wa zamani wa Dynamos FC ya kwao, amewahi pia kuwika timu ya taifa ya nchi hiyo, ingawa kwa sasa hana nafasi tena.
Majabvi aliichezea Zimbabwe kwa mara ya kwanza katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Zambia Julai 15 mwaka 2004 na pia aliiwezesha Dynamos kufika Nusu Fainaali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2008.
Majabvi aliyecheza mechi 14 Ligi ya Mabingwa Afrika na kufunga bao moja dhidi ya timu ya Swaziland mjini Harare, alisajiliwa Dynamos FC mwaka 2006 kutoka Lancashire Steel FC kwa Mkataba wa miaka mitatu.
Mwaka 2007 akiwa Nahodha wa Dynamos FC, aliiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya, Kombe la CBZ na Kombe la Nestle. Alikuwa Nahodha wa kwanza kushinda taji la Ligi Kuu tangu mwaka 1997.
Amekuwa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Zimbabwe mara tatu mwaka 2005 alipokuwa Lancashire Steel na 2007 na 2008 akiwa na Dynamos FC.
Msimu wa 2008–2009, Majabvi alijiunga na Lask Linz FC ya Austria kwa Mkataba wa miaka mitatu kucheza Ligi ya Bundesliga Tipp3 na akang’ara zaidi msimu wa 2011–2012 na tangu ametua Khatoco Khan Hoa FC. mwaka juzi, Majabvi hajawahi kukosa mechi muhimu.
0 comments:
Post a Comment