
Fadhili Omary Sizya,Morogoro.
Waswahili husema biashara asubuhi, jioni mahesabu
hata wengine huongeza kuwa kile unachokipanda ndicho unachokivuna kuhusu maisha
wapo wanaonadi usione mafanikio yanapatikana tambua kuwa mchumia juani hulia
kivulini.
Yote hayo ni maneno ambayo yana maana kubwa sana
katika mzungunguko wa kila siku kwenye maisha ya mwanadamu mpaka pale nafsi
inafikwa na umauti, duniani watu wanakuja kutafuta ,kila aliyewekeza anajenga
jeuri ya alichopandikiza.
Zunguka kila pande za dunia ukitazama sekta ya
michezo kila mmoja amewekeza katika aina tofauti tofauti ambayo huamini hapo
ndipo mafanikio yanapo patikana, wapo wafanyabiashara wakubwa kwa upande wa
mchezo wa soka ambao huamua kuinyanyua timu kwa kuwekeza kupitia kufanya
usajili mkubwa na huamini wanapopata medali za ubingwa,kiasi kikubwa cha
mashabiki ambao wataingia uwanjani ikiwemo uuzwaji mkubwa wa tiketi, bidhaa za
klabu husika zikifanya vizuri sokoni au wamiliki wao binafsi hufikiri kuhusu
kujitengenezea soko ikiwa timu wanazoziendesha zinafanya vizuri, hizo ni baadhi
ya chaguzi za kufanya biashara kwa wamiliki wa timu.
Tukirudi katika ardhi ya nyumbani Tanzania,ukihoji
kuhusu chuo au timu iliyomaarufu kufanya biashara ya wachezaji utaambiwa moja
kwa moja elekea kanda ya Mashariki mkoani Morogoro, funga safari mpaka wilaya
ya Mvomero, kata ya Turiani mtaa wa madizini utafikishwa katika kiwanda cha
Sukari ndani ya Mashamba makubwa ya Miwa utaikuta timu inaitwa Mtibwa Suger.
Ni maarufu watu wa mkoa wa Morogoro hujivunia
matunda yanayolelewa huko na baadaye hao vijana kuwika ndani na nje ya nchi,
mfano ukisikia majina ya kina Nizar Klalfan alicheza yanga, Vancouver Whitecaps
ya Canada,nae Mussa Mgosi kwa sasa meneja wa Simba,Shiza Kichuya mfungaji
mahiri wa kona na mipira iliyokufa pale Simba Sc, Salum Mayanga kocha mkuu wa
Taifa Stars, Meck Meksime kocha mkuu Kagera Suger ni baadhi ya mafanikio ya
kujivunia waliyonayo Mtibwa Suger katika soka nchini hapa.
Wakiwa wanatengeneza vipaji hivyo, bado Mtibwa sio
wazembe katika kupambana kubaki ligi kuu Tanzania, wanaingia katika historia ya
kuwa timu iliyokaa muda mrefu katika michuano hiyo, tangu wapande mwaka 1996
ilipokuwa ilikiitwa ligi daraja la kwanza hawakuwahi kushuka daraja mpaka sasa
wakiwa na mafanikio ya kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo 1999 na mwaka 2000
wakiwa chini ya mwalimu John Simkoko na waliwahi kuubeba ubingwa wa Tusker
mwaka 2008.
Muda wowote kwa sasa ukifika katika kambi ya timu
hiyo wapo wachezaji ambao wapo sokoni, wanafanya vizuri kwa kila mechi
ikiwa ligi inaelekea ukingoni.

Shaban Nditi
Tangu ametua kipindi Mtibwa ipo chini ya kocha
mkongwe John Simkoko ilikuwa mwaka 2000 akitokea mkoani Singida na alifika hapo
kufanya majaribio amedumu mpaka sasa akiwa ni nahodha wa timu hiyo, amekuwa ni
kiungo hodari sana, anasifika kwa nidhamu,kiongozi uwanjani yupo tofauti na
wachezaji wengi uwanjani akibebwa na uwezo wa kuijua miiko ya soka.
Nditi ni tegemezi katika klabu hiyo kwa takribani
misimu yote aliwahi kutamba akiwa na Marcio Maximo katika timu ya taifa kwa
kipindi chote tangu mbrazili huyo alipoteuliwa kuinoa timu hiyo, hachuji
uwanjani, burudani ukimtazama anavyotimiza majukumu yake mara zote amekuwa
akiwashinda uwezo wa kulimiliki dimba wachezaji wengi wa timu za ligi kuu
Tanzania.

Salim Mbonde
Yupo klabuni hapo msimu wa tano sasa ,amekuwa beki
kisiki anategemewa sana kwa utulivu wake katika eneo la ulinzi, ambapo
takribani misimu kadhaa amekuwa akihusishwa kutua katika vilabu vikubwa
Tanzania vikiwemo Simba, Azam na Yanga.
Amekuwa na muendelezo wa kuitwa timu ya taifa na makocha
kwa mihula yote ambao hufundisha Taifa Stars, sasa hivi chini ya Salum Mayanga
bado anatumainiwa akipendwa zaidi kwa uwezo wa kulinda kiwango chake kwa muda
wote.

Said Mohammedi “Nduda”
Aliachwa Yanga baada ya kushindwa kutamba kikosi
cha kwanza, aliandamwa na majeraha kwa misimu kadhaa, aliwika ligi kuu akitokea
Majimaji ya mkoani Songea.
Sasa hivi panga pangua lazima umkute kikosi cha
kwanza labda awe na majeraha ndiyo atakosekana, amejumuishwa Taifa Stars, amekuwa mlinda mlango anayewanyima magoli
wachezaji wengi katika michuano ya ligi kuu, umbo lake zuri la kusimama kulinda
nyavu zake, uwezo wa kuelekeza mabeki wake jinsi ya kujipanga hakika amekuwa
kipa mwenye uwezo wa juu klabuni hapo.

Ally Shomary “Alves”
-Anaweza asiwe na mambo mengi hivyo nadra kufahamika
kwa haraka akiwa yupo uwanjani, amedumu klabuni hapo kwa miaka minne sasa
akicheza fullbeki ya kulia amekuwa imara kwa misimu yote anayotumika klabuni
hapo.
Aliwahi kuhitajika na Simba Sc, ukimuona anavyocheza
utagundua ni hodari kuimudu nafasi yake, anapanda kwa haraka na kurudi kukaba
kwa kasi hiyo hiyo, makocha waliopita kwa kipindi tofauti klabuni hapo akina
Mecky Mekxime, Salum Mayanga na sasa hivi ikinolewa na Zuberi Katwila mara zote
hawana chaguo zaidi ya Ally Shomary.

Mohammed Issa “Mo Banka”
-Huu ni msimu wake wa kwanza akiwa na Mtibwa Suger
akitokea visiwani Zanzibar, lakini ukimtazama anavyolivuruga dimba,akiteleza
kama kambale ni kama amecheza misimu mingi ligi kuu bara au amekaa kikosini
hapo kwa muda mrefu.
Amekuja klabuni hapo kwa kazi mojatu ! ambayo ni kuziba
nafasi walizokuwa wakicheza Mohammed Ibrahim na Mzamiru Yassin waliouzwa Simba
Sc, sasa akisaidiana na kina Ibrahim Jeba, Shaban Nditi amekuwa moto wa kuotea
mbali kwa viungo wengi ligi kuu Bara.

Japhar Salum
Umri wake hauwezi kuzidi miaka 22, ametokea Mtibwa
B anamudu vizuri safu ya ushambuliaji akisimama katikati, binafsi akiwa na
nguvu za kutosha kumiliki mpira lakini anatisha sana baada ya kuwa na watu
wanaomlisha vya kutosha nao wakiwa na kash kasha kina Stamil Mbonde, Said
Bahanuz na hata akipangiwa kucheza na machachari Vicent Barnabas amekuwa hatari
sana anapolitizama lango la timu pinzani.
Sasa hivi amekuwa na manufaa zaidi akiwa na uwezo wa
kupiga mipira ya adhabu, akimudu kuibeba mtibwa tangu mfungaji wao Rashid
Mandawa mwenye mabao 7 akumbwe na majeraha, kijana huyo ameendelea kuonyesha
makali zaidi katika safu ya Ushambuliaji.
0 comments:
Post a Comment