Dar es Salaam,Tanzania.
TIMU ya Simba imepoteza
matumaini ya kuinasa saini ya mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo baada ya jina la mchezaji huyo kuwemo kwenye orodha ya kikosi cha timu yake ya Vital’O kitakachoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo msimu ujao.
Uongozi wa Simba ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili
Zacharia Hanspoppe, uliahidi kumleta Msimbazi mshambuliaji huyo mwenye kulijua vizuri lango la timu pinzani, baada ya kushindwa kufanya hivyo msimu uliopita.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari kutoka Burundi, jina la Mavugo ni miongoni mwa majina 29 ya wachezaji waliosajiliwa na Vital’O,kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo na tayari usajili huo umeshawasilishwa kwenye shirikisho la soka la nchi hiyo, FFB.
Akizungumza jana Hanspoppe alisema walikuwa na mazungumzo na mchezaji huyo pamoja na klabu yake ya Vital’O na wanashangazwa na taarifa hizo za jina lake kuwemo kwenye orodha ya wachezaji watakaoitumikia timu hiyo msimu ujao.
“Inashangaza kusikia taarifa hizo lakini kama Simba hatutakata tamaa
tutaendelea na jitihada zetu za kumsajili kwa kukutana na viongozi wa timu yake na yeye mwenyewe hadi mwisho naamini hakuna kinachoshindikana ukizingatia muda wa usajili bado upo,”alisema Hanspoppe.
Mavugo alikuwa chaguo la kwanza la Simba kwenye usajili wa msimu huu ingawa baadaye miamba ya Kenya, Gor Mahia waliingilia kati mbio hizo nao wakiiwania saini ya Mrundi huyo ambaye ana sifa ya kucheka na nyavu.
0 comments:
Post a Comment